ROHO NYEUPE: Simba ikikosa ubingwa, Aveva na jopo lake wajiuzulu
By GIFT MACHA
Baada ya kuifuatilia timu hiyo kwa muda mrefu sasa nimejiridhisha kuwa kama isipotwaa ubingwa msimu huu rais wa timu hiyo, Evans Aveva na jopo lake la uongozi wanapaswa kubwaga manyanga ili timu hiyo itafute maisha mapya.
KUKUBALI kushindwa sio kosa. Mwanadamu mwenye fikra chanya akiona jambo linamzidi uwezo ama linamtatiza hukubali kuomba msaada kwingine ama kuachana na jambo hilo. Wakati mwingine maisha hayahitaji kulazimisha sana.
Nimekuwa nikifuatilia soka la Tanzania siku hadi siku. Nazifuatilia Simba, Yanga na Azam. Nazifuatilia Majimaji, JKT Ruvu, Stand United na hata Lipuli ambayo inalalamikiwa kuwa inataka kupanda Ligi Kuu kwa njia ya mkato. Kwa kifupi nafuatilia kila eneo.
Hata hivyo, leo sitaki kuzungumzia soka lote, nataka kuijadili Simba. Baada ya kuifuatilia timu hiyo kwa muda mrefu sasa nimejiridhisha kuwa kama isipotwaa ubingwa msimu huu rais wa timu hiyo, Evans Aveva na jopo lake la uongozi wanapaswa kubwaga manyanga ili timu hiyo itafute maisha mapya.
Yawezekana Aveva ni kiongozi bora. Yawezekana jopo lake la uongozi linaundwa na watendaji wenye weledi mkubwa, lakini kama atashindwa kuiongoza timu hiyo kutwaa taji la Ligi Kuu ama la FA ni wazi kuwa wote wanapaswa kuachia ngazi. Hicho ndicho kitu pekee wanachotakiwa kukifanya mwishoni mwa msimu na inaweza kuwajengea heshima Msimbazi kuliko kuendelea kubaki.
Ifahamike kuwa tangu Aveva na wasaidizi wake wamechaguliwa kuongoza Simba mwaka 2014, timu hiyo imeshinda taji moja, ni lile la Mapinduzi mwaka 2015. Simba haijawahi kumaliza katika nafasi hata ya pili Ligi Kuu chini ya uongozi wa Aveva. Hakuna mafanikio ya uwanjani ambayo Aveva na jopo lake wanaweza kujivunia mpaka sasa.
Msimu huu ulionekana kama unaweza kuwa wa neema kwa timu hiyo, lakini mambo ni kama yanaanza kuwa magumu. Simba baada ya kucheza mechi 13 bila kupoteza, maisha yake yamebadilika ghafla na sasa haina uhakika tena wa kushinda mechi.
Licha ya Simba kutengeneza wigo wa pointi nane na Yanga iliyokuwa katika nafasi ya pili, timu hiyo tayari imeshushwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu na inashika nafasi ya pili. Hofu ya kubadilika kwa upepo huo ndani ya muda mchache inazua hofu kama ni kweli Simba inaweza tena kupindua meza na kushinda taji hilo.
Yawezekana uongozi ukajivua lawama kwa madai kuwa benchi la ufundi la timu hiyo ndio linapaswa kulaumiwa, lakini hilo haliondoi ukweli kwamba utendaji wao utakuwa umefikisha miaka mitatu bila kuleta mabadiliko yoyote ya maana.
Kama unakuwa rais wa timu kwa miaka mitatu na timu yako haijashinda taji lolote la maana. Timu yako haijapata tiketi yoyote ya uwakilishi wa michuano ya kimataifa, uongozi wako una thamani gani? Unakuwa kiongozi unayewaongoza watu kuelekea wapi? Motoni? Sidhani!
Matatizo yanayoikumba Simba sasa hasa katika safu yao ya ushambuliaji yanatokana na uongozi kushindwa kufanya kazi yao vizuri, hasa kamati ya usajili. Ikumbukwe kuwa Kocha Joseph Omog alipendekeza timu hiyo isajili straika mwenye uwezo wa juu ili kuimarisha safu hiyo ambayo tayari ilikuwa inasuasua chini ya Frederick Blagnon na Laudit Mavugo ambao walifunga mabao matano tu katika duru lote la kwanza.
Uongozi wa Simba baada ya kupitia taarifa ya Omog ulifanya kituko kimoja. Ulikwenda kumsajili straika, Pastory Athanas kutoka Stand United ambaye katika duru lote la kwanza alifunga bao moja tu. Huu ni utani uliopitiliza. Huyu ndiye straika wa maana aliyemtaka Omog? Anafahamu Aveva na jopo lake.
Baada ya hapo Simba ikaenda kumsajili kwa mkopo, Juma Liuzio kutoka Zesco ya Zambia. Bahati nzuri wiki moja kabla ya kusajiliwa kwa Liuzio, Mwandishi wa Mwanaspoti, Olipa Assa alifanya makala na mchezaji huyo ambapo alikiri kuwa ana maisha magumu katika kikosi cha Zesco na amekuwa akichezeshwa kwa dakika kati ya 12-15 tu. Kwa msimu wote uliopita akiwa Zesco Liuzio alikuwa amefunga mabao matatu tu. Maneno haya aliyasema kwa kinywa chake na wiki moja baadaye alikamilisha usajili wa kujiunga na Simba. Unajiuliza tena, huyu ndiye yule straika wa kiwango cha juu aliyempendekeza Omog? Utani mwingine huo. Uzuri ni kwamba namba huwa hazidanganyi. Athanas hajafunga bao hata la kuotea katika mechi tano za Ligi Kuu alizoichezea timu hiyo. Straika huyo amefunga bao moja tu dhidi ya timu ya daraja la kwanza, Polisi Dar katika mchezo wa FA. Pengine ndio timu anazoweza kuzifunga.
Liuzio naye hajafunga bao hata la kuotea katika mechi nne za Ligi Kuu alizocheza. Alifunga bao moja pekee katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi. Je huyu ndiye ‘masia’ tuliyeambiwa tumsubiri? Anafahamu Aveva na jopo lake. Katika mazingira kama haya ni wazi kuwa safu hiyo ya uongozi wa Aveva kama haitafanya juhudi za kupata tiketi ya mashindano ya kimataifa ama kushinda ubingwa, haipaswi kuendelea kuiongoza Simba. Itakuwa ni muda muafaka kupeana mkono wa kwaheri.
0 comments:
Post a Comment