.

.

Sunday, 19 July 2015

Mshambuliaji wa Yanga, Kpah Sherman (kushoto) akiwania mpira na mchezaji wa Gor Mahia ya Kenya, Collins Okoth wakati wa mchezo wa Kombe la Kagame kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam jana. Yanga ilifungwa 2-1. (Picha na Rahel Pallangyo).MA B I N G W A wa Tanzania Bara, Yanga, jana walianza vibaya mashindano ya Afrika Mashariki na Kati ya Kombe la Kagame, baada ya kuchapwa mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Gor Mahia ambayo nusura ishindwe kushiriki mashindano hayo kutokana na ukata na kuokolewa na serikali ya nchi yao, ilipata ushindi huo mbele ya Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga.
Wenyeji Yanga ndio walikuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza katika dakika ya nne lililofungwa na mchezaji wa Gor Mahia, ambaye alitaka kuokoa mpira uliopigwa na Donald Ngoma na kuujaza wavuni.
Gor Mahia ilicharuka na kusawazisha muda mfupi baadae kwa bao la Michael Olunga alilofunga kwa kichwa baada ya kuruka kuwazidi mabeki wa Yanga na kujaza mpira wavuni.
Yanga ilipata pigo katika dakika ya 11 baada ya kutolewa kwa mchezaji wake Mzimbabwe Ngoma, kutokana na kumsukuma beki wa Gor Mahia.
Huku wakishangiliwa na mashabiki wanaodhaniwa kuwa ni wa Simba, Gor Mahia walipata bao katika dakika ya 46 lililofungwa tena na Olunga baada ya kuwatoka mabeki wa Yanga na kuujaza mpira wavuni kulia kwa kipa Mustapha.
Wachezaji wa Gor Mahia waligoma kuingia katika vyumba vya kubadilishia nguo, ambapo walitumia mlango tofauti. Yanga walipata penalti baada ya mchezaji mmoja wa Gor Mahia kuunawa mpira lakini nahodha wa Yanga,Nadir Haroub alipiga mpira na kuokolewa na kipa Boniface Oluoch.
Yanga iko katika kundi A pamoja na Gor Mahia, Telecom (Djibout), KMKM (Zanzibar) na Khartoum-N (Sudan) wakati Kundi B linaundwa na timu za APR (Rwanda), Al-Shandy (Sudan),LLB AFC (Burundi) na Heegan FC (Somalia).
Kundi C lina timu za Azam FC (Tanzania), Malakia (Sudan Kusini), Adama City (Ethiopia) na KCCA (Uganda).
Vikosi Yanga ilianza na:- Ally Mustafa Barthez, Amiss Tambwe, Nadir Haroub, Mbuyi Twitte, Simon Msuva, Juma Abdul, Deus Kaseke, Haruna Niyozima, Kelvin Yondan, Mwinyi Haji na Donald Ngoma
Gor Mahia: Boniface Oluoch, Karim Nizigiyimana, Mussa Mohammed, Haron Shakava, Abouba Sibomana, Innocent Wafura, Diikir Glay, Kharid Aucho, Godfrey Walusimbi, Michael Olunga na Meddie Kagere, Michuano hiyo itaendelea tena leo kwa Azam FC kucheza na Katika mchezo wa awali kwenye mashindano hayo, APR ya Rwanda iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Al Shandy ya Sudan.
Katika Uwanja wa Karume, KMKM ya Zanzibar iliibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo mwingine wa michuano hiyo dhidi ya Telecom ya Djibout.

0 comments:

Post a Comment