
BAADA ya kutoweka hadharani tangu Julai 28, mwaka huu, Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk Wilbrod Slaa amejitokeza hadharani na kuelezea
kilichomsibu, akiweka wazi kwamba amestaafu siasa baada ya chama hicho
kumpokea aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa ambaye amesisitiza hawezi
kukwepa kashfa ya Richmond.
Dk Slaa aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano uliodumu kwa
takribani saa mbili katika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam jana kuwa
Lowassa si kiongozi anayefaa kuwa rais wa nchi kutokana na kuhusika na
vitendo vya rushwa na kwamba ni mhusika namba moja katika kashfa ya
Richmond, iliyomwondoa madarakani Februari 2008. Tangu Julai 28, wakati
Lowassa alipoanza kuonekana katika vikao vya Chadema, Dk Slaa amekuwa
haonekani katika vikao vya chama hicho ikiwemo Mkutano Mkuu uliomtangaza
Lowassa kuwa mgombea urais wa chama hicho na umoja wa wapinzani (Ukawa)
katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Mbali ya Mkutano Mkuu, Dk Slaa hakuonekana katika matukio muhimu kama
yale ya Lowassa kufika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchukua fomu ya
kugombea urais na wakati wa kuirejesha, na pia katika mkutano wa
uzinduzi wa kampeni kwenye Viwanja vya Jangwani, Agosti 29, mwaka huu.
Katika mkutano wa jana, Dk Slaa alieleza kwa kirefu kilichotokea na
kumfanya kupotea katika harakati za Chadema huku akiweka wazi kuwa ujio
wa Lowassa ulimfanya ajiuzulu nafasi ya Ukatibu Mkuu, tofauti na madai
ya Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe kwamba alikuwa likizo. “Nimejitokeza
leo, mimi sikuwa likizo.
Mengi yamesemwa na viongozi wangu, lakini ukweli ni kwamba sikupewa
likizo na yeyote, nasisitiza sina barua yoyote ya likizo. “Kilichotokea
ni kwamba niliamua kuachana na siasa tangu tarehe 28/7 majira ya saa 3
usiku, baada ya kuona yanayofanyika ndani ya chama changu na
sikukubaliana nayo,” alisema Dk Slaa na kuongeza: “Wapo watu wanaosema
Dk Slaa alishiriki kutoka mwanzo katika ujio wa Lowassa.
Nilishiriki kweli, lakini niliweka msingi tangu dakika ya kwanza
kutaka kujua Lowassa anakuja Chadema kama mali au anakuja kama mzigo?
Msimamo wangu huu haukupatiwa majibu na hadi sasa viongozi wa Chadema
hawana majibu katika hili.”
Akisimulia mkasa mzima, padri huyo wa zamani wa Kanisa Katoliki
alisema baada ya Lowassa kukatwa kwenye mchakato wa kumpata mgombea
urais kupitia CCM mjini Dodoma, alipigiwa simu na Askofu wa Kanisa la
Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima aliyemwita kuwa mshenga wa Lowassa,
akimuarifu hatua hiyo ya kukatwa Lowassa ni mtaji kwa Chadema.
Alisema katika maelekezo yake, Askofu Gwajima alimuelekeza Dk Slaa
awasiliane na Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe kuhusu mpango huo na
kumrejeshea majibu ya kile walichoafikiana na kwamba alitekeleza ombi
hilo kwa kuwasiliana na Mbowe na baadaye walimkaribisha Askofu Gwajima
ili kuzungumza kwa kina.
“Tangu wakati huo niliweka msimamo wangu. Unajua kwa kawaida ni
vizuri kumsikia mtu ana nini na si kutomsikiliza kabisa. Chadema ni
chama cha siasa haikatazwi kumpokea mtu. “Niliweka msimamo kwanza
atangaze kutoka ndani ya CCM, baada ya kutangaza hilo atangaze pia ni
chama gani anakwenda, halafu tatu atumie nafasi hiyo kujisafisha na
tuhuma zake anazoshutumiwa.
Niliweka msimamo huo kwa kuamini kuwa Chadema ni chama kilichojijenga
katika misingi ya uadilifu na iwapo asingefanya hivyo ni hatari,”
alifafanua Dk Slaa aliyegombea urais kwa chama hicho mwaka 2010. Alisema
kinyume cha msimamo aliouweka, Lowassa hakutangaza kujitoa CCM na
kutangaza anakwenda chama gani kwa wakati huo, lakini pia hakujisafisha
hadi alipokuwa katika kikao cha utambulisho Chadema ndipo alipozungumzia
suala la Richmond baada ya kuulizwa na waandishi wa habari tena katika
hali ya udikteta.
Alisema mbali ya msimamo huo, aliweka msimamo mwingine wa kutaka
kujua, Lowassa anakwenda Chadema akiwa ni mali au mzigo, katika kile
alichosema ilikuwa ni kutaka kutathmini kama ujio huo wa Lowassa kwa
Chadema ungekuwa na manufaa au hasara. “Ujue kwenye biashara au siasa,
anayejiunga leo ni lazima mfahamu, je, anakuja kama mali au kama mzigo?
Watu hapa wanasema nilipatwa na hasira kwa vile alipewa nafasi ya
kugombea urais, suala si urais, hadi siku hiyo nilikuwa sijachukua fomu
ya urais, kama ningekuwa nataka urais ningetangaza au kuchukua fomu
kwani jina langu lilishapitishwa na vikao tangu Februari. “Hapa ukweli
ni kwamba Slaa alikuwa anataka mgombea mwenye uwezo, sifa na anayeweza
kuivusha Chadema kuiondoa CCM.
Hata mwaka 2010 sikujitokeza mimi kugombea urais, bali niliombwa.
Urais si wangu, mimi binafsi ni kwa ajili ya watu,” alieleza akifafanua
madai hayo ya kuwa alikasirika kwa kutoteuliwa kuwania urais. Alisema
kutokana na swali hilo, alijibiwa kwamba Lowassa angekwenda Chadema na
wabunge 50 waliokuwa wakimaliza muda wao, wenyeviti wa CCM wa mikoa 22,
wenyeviti wa CCM wa wilaya 88, na hivyo aliamini kama ingekuwa hivyo
nchi ingeweza kutetemeka.
“Niliweka sharti majina yatajwe, nilifanya vile kwa kuwa Katibu Mkuu
makini wa chama hawezi kupokea tu watu, bila kujua ni akina nani na
wanagombea wapi maana tulikuwa tayari na mfumo wa kuwaandaa wagombea
ndani ya chama, hata hivyo majina hayo sikuyapata. Alisema ilipofika
Julai 25, kilifanyika kikao ambacho aliagizwa kuitisha kikao cha
Halmashauri Kuu na alipohoji nini kinaenda kuzungumzwa, hakupewa jibu.
Alisema Julai 25, alipigiwa simu na Mbowe ambapo katika mazungumzo
yao kwa mara ya kwanza walitofautiana, ingawa alikubali kufika katika
kikao alichowakuta Mbowe, Askofu Gwajima na Mwanasheria wao, Tundu
Lissu. “Kikao kile kilianza saa 3 asubuhi hadi saa 9 jioni, na
tulibishana sana, maana swali langu lilibakia kuwa lile lile, je Lowassa
anakuja Chadema kama mali au kama mzigo?
Baada ya pale walisema twende nyumbani kwa Lowassa, lakini nilikataa
kwani Lowassa ni mwanachama wa CCM hivyo mimi nisingeweza kwenda.
“Tulirejea tena katika kikao kuanzia saa 9 jioni hadi saa 12.30,
tukapumzika, lakini hatukuelewana. Wakaunda kamati ndogo ya kuzungumza
na mimi na kunishauri, lakini nilikataa. Pale pale niliandika barua ya
kujiuzulu nikampa Mwenyekiti wa kikao, Profesa Safari (Abdalah) lakini
aliichana pale pale.
“Sikuridhika na hatua hiyo niliandika barua nyingine na kumkabidhi
Makamu Mwenyekiti wa Zanzibar ambaye alinijibu kwamba Dk Slaa
unajisumbua bure haya mambo yamepangwa. Hata hivyo, kesho yake
niliandika barua rasmi ya kujizulu,” alieleza kiongozi huyo
aliyeheshimika kwa misimamo yake ndani ya Chadema.
Akizungumzia nini kilifuata baada ya Lowassa kupokelewa Chadema;
alisema alikwenda kama mzigo na si mali kwani yeye na wafuasi wake ni
watu ambao ama walikataliwa na wananchi katika kura za maoni, au ni
ambao wamekuwa wakituhumiwa katika masuala ya ufisadi na hawawezi
kukubalika ndani ya jamii.
“Awali niliweka msimamo kwamba wale watakaokuja na Lowassa ni vizuri
waje kabla ya kufanyika kura ya maoni, hilo halikuzingatiwa. Dk Mahanga
(Makongoro, aliyekuwa Mbunge wa Ukonga na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira)
huyo ni mali au ni mzigo? Huyo amekataliwa na wananchi hivyo alikuwa
anatafuta kichaka cha kujificha. “Hivi Sumaye (Frederick, Waziri Mkuu
mstaafu) huyo ni mtu safi kweli. Watu wote wanamfahamu kwamba ni fisadi.
Nilimwita fisadi ndani ya Bunge wakati ule alipopokonya shamba la
Magereza Kibaigwa. “Huyu Sumaye ndiye ambaye alisema CCM ikimteua
Lowassa atahama chama. Watu wote mnajua Sumaye alikuwa anaitwa nani
wakati ule… (kicheko). Leo makapi yametoka CCM yamekwenda Chadema.
Wenyeviti waliondoka ni mizigo, wote tunamjua Msindai (Mgana,
aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida na Mwenyekiti wa Wenyeviti
wa CCM). “Mimi namfahamu Msindai, alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu
za Serikali kabla yangu pale Bungeni alichokifanya ipo siku nitamuweka
hadharani.
Mtu ambaye siwezi kumsema ni Mgeja (Khamis, aliyekuwa Mwenyekiti wa
CCM wa Mkoa wa Shinyanga)… huyo siwezi kumsema maana simfahamu,”
alieleza Dk Slaa. “Kuna mtu anaitwa Chizi, hivi Chizi ni nani?
Nilipofuatilia ili kumjua vizuri nikaambiwa eti alikuwa anapanga mipango
ya wizi wa kura ndani ya CCM.
Yaani Chadema inampokea mtu kwa vile tu alikuwa mwizi wa kura? Kama
tunataka Chadema kuiba kura kuna umuhimu gani wa kuiondoa CCM
madarakani? Unaiondoa CCM kwa programu safi serious (makini) na watu
serious (makini).”
Kuhusu Richmond, Dk Slaa alisema bado anaamini kuwa Lowassa hawezi
kukwepa kashfa hiyo na alionesha na kusoma vielelezo na barua
mbalimbali, alizosema zinadhihirisha Lowassa kuwa mpangaji mkuu wa
mpango wa ufisadi wa Richmond na kwamba kupokelewa na Chadema,
kumekifanya chama hicho kupoteza nguvu ya hoja ya kupambana na ufisadi,
hoja aliyosema ilikuwa silaha pekee kwa Chadema.
Dk Slaa alimtaka Waziri Mkuu huyo wa zamani, kujitokeza na kueleza
namna alivyohusika na sakata la Richmond, kwa kutaja Richmond ilikuwa
kampuni ya nani, na ni wakubwa gani walioshinikiza kutolewa kwa zabuni
hiyo ya kufua umeme wa dharura kama alivyodai na kuahidi kutoa taarifa
zaidi ya umma kwa suala hilo.