MGOMBEA wa urais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kupitia Chadema,
Edward Lowassa, amesema haitoshi kwa watu kuendelea kufurika katika
mikutano yake pasipo kutia nia ya kumpigia kura ili aweze kuwa Rais wa
Serikali ya Awamu ya Tano.
Lowassa anayeungwa mkono na vyama vingine vitatu vya CUF, NCCR-
Mageuzi na NLD, alisema umati wa watu wanaojitokeza kumsikiliza kila
mahali ikiwemo Morogoro Mjini hakutoshi iwapo hawataweza kumpigia kura
nyingi za kuingia madarakani Oktoba 25, mwaka huu.
Lowassa aliyekuwa Waziri Mkuu wa kwanza katika Serikali ya Awamu ya
Nne na kulazimika kuachia madaraka mapema mwaka 2008, alihutubia
takribani kwa dakika kumi na baadaye kuwakaribisha na kuwatambulisha
wagombea wa ubunge wa Jimbo la Morogoro Mjini na madiwani wa Kata
mbalimbali ili kuwaombea kura kwa wananchi.
Alianza ziara yake kwa kuwahutubia wananchi wa kata ya Dumila,
Turiani na kuwasili mjini Morogoro jioni ya saa kumi akiambatana na
aliyekuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye
ambaye kama Lowassa, amejiengua CCM baada ya kukataliwa kuwania urais
kwa tiketi ya chama hicho tawala.
Akihubutia katika mkutano huo uliofanyika katika uwanja wa Shule ya
Msingi Kiwanja cha Ndege, Manispaa ya Morogoro, alisema mahudhurio hayo
na kumshangilia huko kwa wingi kuonekane pia katika sanduku la kura.
Pia alitumia muda huo kuelezea azma yake endapo wananchi watamchagua
kuwa Rais wa Tanzania, ataangalia namna ya kufufua viwanda vya Morogoro
na ikiwezekana kuanzisha vipya ili kuwezesha upatikanaji wa ajira na
kuuza bidhaa ghafi nje badala ya kuuza malighafi kama ilivyo kwa sasa.
Alisema, si dhambi viwanda kuendeshwa na serikali kwa kuwa jambo hilo
linafanyika hata katika nchi nyingine za Ulaya na kutolea mfano
Ufaransa ambako baadhi ya viwanda na mabenki yanamilikiwa na serikali.
Hivyo aliwataka wananchi kuwapigia kura wagombea wa Chadema kwa
nafasi ya udiwani, ubunge ili aweza kupata timu atakayofanya nayo kazi
endapo atachaguliwa kuwa rais.
Pamoja na hayo, alisema serikali yake atakayoiunda itakuwa rafiki wa
mama lishe, bodaboda na wamachinga na kwamba ataanzisha benki
itakayoshughulikia makundi hayo.
Pia alisema serikali yake itasimamia uboreshaji wa elimu, maslahi ya
walimu na kutoa elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi chuo kikuu na
kwamba endapo ataingia madarakani wanafunzi wote watasomba bure bila
kulipa michango.
Wednesday, 16 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment