MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli ameahidi
kunyang’any’a mashamba ambayo yamehodhiwa na watu bila kutumiwa kwa
ufugaji wala kilimo, na kuyagawa kwa wakulima na wafugaji wasio na
maeneo ya kilimo. Alisema hayo alipozungumza na wananchi wa wilaya za
Ulanga na Kilombero mkoani Morogoro jana.
Dk Magufuli alisema akiwa rais, kuna mambo mengi anaweza kufanya,
kukabiliana na migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji na
mojawapo ni kutoa ardhi zaidi kwaajili ya wakulima na wafugaji, ili
kuondoa uhaba wa ardhi, unaosababisha ugomvi wa maeneo ya kulishia
mifugo na kulima.
Alisema kuna watu wanamiliki maelfu ya eka za ardhi bila kulima na
kwamba atanyang’any’a mashamba hayo ambayo yamehodhiwa na watu hao bila
kutumiwa kwa ufugaji wala kilimo. Akihutubia maelfu ya wananchi, pia Dk
Magufuli alisema kuwa anajivunia uzoefu wa marais wastaafu wa Awamu ya
Pili mpaka Awamu ya Nne na wa Zanzibar, kwamba ndio atakaowafuata kwa
ushauri akikwama popote.
Alisema hiyo ni moja ya tofauti kubwa kati yake na wagombea wengine
wa urais. “Nitaingia Ikulu nikiwa na washauri wazuri, nikikwama mahali
nitakwenda kwa Rais Jakaya Kikwete, nikikwama nitaenda kwa mzee Benjamin
Mkapa, nikikwama tena nakwenda kwa mzee Ali Hasan Mwinyi.
“Wako wengi, upo ushauri nitauchukua kutoka kwa mzee Salmin Amour
(Rais Mstaafu wa Zanzibar), Dk Ali Mohamed Shein na kwa Amani Abeid
Karume,” alisema. Kutokana na fursa hiyo ya kiuongozi aliyonayo ndani ya
Chama Cha Mapinduzi, Dk Magufuli aliomba Watanzania wote bila kujali
vyama vya siasa, makabila wala dini kumpa kura kwa wingi kwa kuwa
atakuwa na washauri wazuri wenye uzoefu.
Alisema wagombea wengine, akiwemo wa Chadema anayeungwa mkono na
vyama vinavyounda Ukawa, Edward Lowassa, hawataweza kupata ushauri wa
washauri hao kama ilivyo rahisi kwake.
Kutokana na uhakika huo wa washauri wazoefu, Dk Magufuli alisema ndio
maana baadhi ya wagombea hao wanaweza kuja na ahadi za uongo, ikiwemo
ya kuondoa nyumba za tembe na za nyasi.
Aliwataka wananchi kuwapima wagombea hao katika ahadi zao, kwa kuwa
baadhi walikuwepo ndani ya Serikali kwa muda mrefu, lakini walishindwa
kuondoa nyumba hizo katika majimbo walikotokea.
Dk Magufuli alisema yeye hataahidi kuondoa nyumba hizo, bali anaahidi
kushusha bei ya vifaa vya ujenzi hasa saruji, mabati na misumari, ili
wananchi wanaofanya kazi wajenge nyumba bora.
Katika kuongeza idadi ya Watanzania wanaofanya kazi ili kufikia lengo
hilo, Dk Magufuli alisema katika kila mtaa na kijiji, serikali yake
itatoa Sh milioni 50 kwa ajili ya kuanzisha na kukuza biashara ndogo za
wanawake na vijana.
Alisema atataka kila anayefanya kazi apate kipato kizuri
kitakachomsaidia kukabiliana na mahitaji ya maisha yake, ikiwemo kujenga
nyumba bora kutokana na kushushwa kwa bei za bidhaa za ujenzi. Kwa
wakulima, alisema atahakikisha pembejeo sahihi zinatolewa kwa wakati na
mazao yatakayovunwa, itakuwa marufuku kwa Serikali kukopa mazao yao.
Saturday, 5 September 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment