.

.

Wednesday, 2 September 2015

MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli amesema Serikali atakayoiongoza baada ya kuchaguliwa, itapandisha mishahara ya watumishi wote wa umma ilingane na ile ya Wakala wa Taifa wa Barabara (Tanroads), ambayo aliianzisha na kuwapa wafanyakazi wake mishahara minono.
Hata hivyo, Dk Magufuli alisema baada ya kuongeza mishahara hiyo, wafanyakazi lazima wachape kazi na kuonya kuwa wasipofanya hivyo atapambana nao. Aidha, amesema Serikali atakayoiongoza, itapunguza bei ya vifaa vya ujenzi, hasa saruji na mabati.
Alisema hayo jana katika mikutano midogo aliyofanya njiani alikokuwa akisimamishwa na wananchi wakati alipokuwa akitoka Songea, kupitia Namtumbo na Tunduru kwenda Masasi mkoani Mtwara.
Dk Magufuli alisema mkoani Mtwara tayari ujenzi umeanza wa kiwanda cha saruji ambacho ndio kikubwa kuliko vyote Afrika Mashariki na Kati na kikikamilika, kitazalisha saruji nyingi na kupunguza bei ya bidhaa hiyo muhimu ya ujenzi.
Alisema kusudio la kushusha bei ya vifaa hivyo ni kusaidia wananchi wajenge nyumba nzuri na bora za makazi kwa ajili ya kuboresha maisha yao. Kuhusu kuboresha kipato cha wananchi ili wafanikishe azma ya kutumia punguzo la bei za bidhaa za ujenzi na kujenga nyumba bora, Dk Magufuli alisema umeme umeanza kufika katika maeneo hayo na Serikali yake itahakikisha vijijini kunajengwa viwanda vidogo vitakavyotoa ajira vijijini.
Mbali na ajira, pia aliahidi kutoa Sh milioni 50 kwa kila kijiji na kila mtaa, kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza miradi midogo midogo ya kujipatia kipato kwa ajili ya wanawake na vijana.

0 comments:

Post a Comment