
NAHODHA wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars, Nadir Haroub amesema
leo watafia uwanjani mjini Algiers katika mechi ya kuwania kufuzu
michuano ya Kombe la Dunia Urusi 2018 watakaporudiana na wenyeji
Algeria.
Stars inaingia uwanjani leo ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya
mabao 2-2 dhidi ya vigogo hivyo vya Afrika katika mechi ya kwanza
iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam mwishoni mwa wiki
iliyopita.
Katika mechi hiyo, Stars ilikuwa mbele kwa mabao 2-0 mpaka dakika ya
71 ndipo Algeria wakapata mabao ya harakaharaka na kuondoa furaha
miongoni mwa watanzania waliofurika uwanjani siku hiyo.
Matokeo hayo yanaifanya Stars ihitaji ushindi katika mechi ya leo au
sare ya kuanzia mabao 3-3 ili kujihakikishia kukata tiketi ya kucheza
hatua ya makundi ya michuano hiyo, ambayo ni ya mwisho kabla ya kufuzu
kucheza fainali za Kombe la Dunia.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya mtandao jana, Haroub alisema
anaamini timu yake inaweza kuibuka na ushindi ugenini leo. “Soka
imebadilika sana siku hizi, ile ya miaka ile sio ya leo lolote linaweza
kutokea kesho (leo) na tukasonga mbele, mbona hao Algeria tulienda nao
sawa tu mechi ya kwanza makosa madogo tu yamefanyika wakasazisha lakini
tunao uwezo wa kuwafunga,” alisema.
Mashabiki wa timu ya taifa, Taifa Stars, bado wana taharuki ya
matokeo ya sare ya 2-2 dhidi ya Algeria, lakini nahodha wa Stars, Haroub
ametamka kishujaa kuwa kazi haijaisha na anaamini timu hiyo itafanya
makubwa kutokana na safu kali ya ushambuliaji waliyonayo.
“Mimi naamini kabisa timu yetu ipo vizuri kila sehemu nawaambieni
washambuliaji wangu kwamba watatubeba katika mechi hiyo bila shaka
yoyote,” alisema. Safu ya ushambuliaji ya Stars inaongozwa na wachezaji
Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaocheza soka ya kulipwa TP Mazembe
ya Congo DR.
Haroub ambaye pia ni nahodha wa mabingwa wa soka Bara, Yanga, alisema
Stars itawashangaza wengi leo kama ilivyokuwa kwenye mechi iliyopita.
“Mechi iliyopita hakuna aliyetarajia tungepata bao hata moja lakini
matokeo yake tulifunga mabao mawili mpaka waarabu (Algeria) wenyewe
walichanganyikiwa, hivyo hata huku inawezekana tu kushinda,” alisema.
Awali, kabla ya safari ya Algiers juzi, kocha mkuu wa timu hiyo
Charles Mkwasa alisema anatarajia timu yake kupata matokeo mazuri.
Mkwasa alikiri kufanya makosa ya kiufundi wakati wa mabadiliko katika
mechi hiyo lakini akasema hiyo ni hali ya mpira hutokea mara nyingi.
Katika mechi hiyo ,Mkwasa aliwatoa Mudathir Yahya na Elias Maguli na
nafasi zao kuchukuliwa na Said Ndemla na Mrisho Ngassa, mabadiliko
ambayo hayakuwa na faida kwa timu, jambo lililofanya wapinzani wao
kusawazisha mabao hayo mawili ndani ya dakika nne.
“Makosa hutokea kwenye mpira, ni jambo la kawaida nasi safari hii
tumekutana na makosa hayo, benchi la ufundi imeyaona itayafanyia kazi
yasijirudie katika mechi ya marudiano,” alisema Mkwasa.