.

.

Tuesday, 17 November 2015

NAHODHA wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars, Nadir Haroub amesema leo watafia uwanjani mjini Algiers katika mechi ya kuwania kufuzu michuano ya Kombe la Dunia Urusi 2018 watakaporudiana na wenyeji Algeria.
Stars inaingia uwanjani leo ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya vigogo hivyo vya Afrika katika mechi ya kwanza iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita.
Katika mechi hiyo, Stars ilikuwa mbele kwa mabao 2-0 mpaka dakika ya 71 ndipo Algeria wakapata mabao ya harakaharaka na kuondoa furaha miongoni mwa watanzania waliofurika uwanjani siku hiyo.
Matokeo hayo yanaifanya Stars ihitaji ushindi katika mechi ya leo au sare ya kuanzia mabao 3-3 ili kujihakikishia kukata tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo, ambayo ni ya mwisho kabla ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya mtandao jana, Haroub alisema anaamini timu yake inaweza kuibuka na ushindi ugenini leo. “Soka imebadilika sana siku hizi, ile ya miaka ile sio ya leo lolote linaweza kutokea kesho (leo) na tukasonga mbele, mbona hao Algeria tulienda nao sawa tu mechi ya kwanza makosa madogo tu yamefanyika wakasazisha lakini tunao uwezo wa kuwafunga,” alisema.
Mashabiki wa timu ya taifa, Taifa Stars, bado wana taharuki ya matokeo ya sare ya 2-2 dhidi ya Algeria, lakini nahodha wa Stars, Haroub ametamka kishujaa kuwa kazi haijaisha na anaamini timu hiyo itafanya makubwa kutokana na safu kali ya ushambuliaji waliyonayo.
“Mimi naamini kabisa timu yetu ipo vizuri kila sehemu nawaambieni washambuliaji wangu kwamba watatubeba katika mechi hiyo bila shaka yoyote,” alisema. Safu ya ushambuliaji ya Stars inaongozwa na wachezaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaocheza soka ya kulipwa TP Mazembe ya Congo DR.
Haroub ambaye pia ni nahodha wa mabingwa wa soka Bara, Yanga, alisema Stars itawashangaza wengi leo kama ilivyokuwa kwenye mechi iliyopita. “Mechi iliyopita hakuna aliyetarajia tungepata bao hata moja lakini matokeo yake tulifunga mabao mawili mpaka waarabu (Algeria) wenyewe walichanganyikiwa, hivyo hata huku inawezekana tu kushinda,” alisema.
Awali, kabla ya safari ya Algiers juzi, kocha mkuu wa timu hiyo Charles Mkwasa alisema anatarajia timu yake kupata matokeo mazuri. Mkwasa alikiri kufanya makosa ya kiufundi wakati wa mabadiliko katika mechi hiyo lakini akasema hiyo ni hali ya mpira hutokea mara nyingi.
Katika mechi hiyo ,Mkwasa aliwatoa Mudathir Yahya na Elias Maguli na nafasi zao kuchukuliwa na Said Ndemla na Mrisho Ngassa, mabadiliko ambayo hayakuwa na faida kwa timu, jambo lililofanya wapinzani wao kusawazisha mabao hayo mawili ndani ya dakika nne.
“Makosa hutokea kwenye mpira, ni jambo la kawaida nasi safari hii tumekutana na makosa hayo, benchi la ufundi imeyaona itayafanyia kazi yasijirudie katika mechi ya marudiano,” alisema Mkwasa.

0 comments:

Post a Comment