MKUU
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki amemuomba mmiliki wa
Kampuni ya Q Consult inayomilikiwa na mfanyabiashara Yussuf Manji
kutumia busara kukubali kuuachia ufukwe wa Coco jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Sadiki
alisema Mahakama Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Ardhi katika uamuzi wake
imeiamuru Manispaa ya Kinondoni, kutekeleza mkataba wake na kampuni ya Q
Consult kwa ajili ya kampuni hiyo kuendeleza ufukwe huo hata hivyo
Manispaa ya Kinondoni imekata rufaa.
“Kampuni ya Q Consult kwa busara tu iachane na kesi, ikubali
kurudisha ufukwe huo chini ya mamlaka ya Kinondoni ili iweze kuuendeleza
ufukwe huo kwa manufaa ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam na sio kwa
manufaa ya mtu mmoja kama anavyotaka mtu huyo,” alisema Sadiki.
Alisema wananchi wafahamu kuwa ufukwe huo wa Coco haujauzwa, kama
watu wanavyodai na kwamba kesi hiyo iko mahakamani, ambapo Ofisi ya
Manispaa ya Kinondoni kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali wamekata
rufaa.
Akielezea sakata hilo, Sadiki alisema kampuni ya Q Consult
inayomilikiwa na Manji mwaka 2007 iliingia mkataba na Manispaa ya
Kinondoni kuendeleza ufukwe huo.
Alisema, hata hivyo, baadaye Manispaa ya hiyo ilivunja mkataba huo
baada ya Kampuni ya Q Consult kushindwa kutimiza masharti, jambo ambalo
liliifanya kampuni hiyo kwenda mahakamani.
Mahakama Kuu ya Tanzania Kitengo cha Ardhi iliamuru Manispaa ya
Kinondoni, kutekeleza mkataba wake na kampuni hiyo kwa ajili ya
kuendeleza ufukwe huo.
“Kama nilivyosema kupitia mwanasheria mkuu wa Serikali tumekata rufaa
katika uamuzi huo kwasababu tunaamini haukuwa sahihi, hata hivyo
mwekezaji huyo namshauri tu anaweza kufanya maamuzi akaachana na kesi
hiyo na kuamua kurudisha ufukwe huo uendelee kutumiwa na Watanzania
wote,” alisema Sadiki.
Kwa kampuni hiyo kushinda kesi hiyo, inamaanisha kuwa mwekezaji huyo
endapo ataendeleza eneo hilo, wananchi hawatakuwa na fursa hiyo tena,
kama wanavyoutumia sasa.
Sadiki alisema tayari serikali imefanya mazungumzo na moja na benki
hapa nchini kwa ajili ya kupata mkopo, ambao utasaidia kuendeleza eneo
hilo ili liendelee kubaki chini ya Manispaa ya Kinondoni na kutumiwa na
watu wote.
Sunday, 6 December 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment