KATIBU wa Mila wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, Mwanasimtwa
Mwagongo amesema tukio la kupatwa kwa jua linalotarajiwa kutokea leo
katika Kijiji cha Rujewa wilayani hapa ni ishara ya Mwenyezi Mungu
kuukubali uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John
Magufuli.
Hii itakuwa ni mara ya kwanza Tanzania kutokea tukio hilo tangu
Aprili 18, 1977 na kwamba tukio kama hilo la kihistoria linatarajiwa
kutokea tena nchini Mei 21, 2031.
Mbali ya Rujewa ambako wataona kupatwa kwa jua kwa asilimia 97 sawa
na miji ya Makambako, Masasi, Mbeya, Tunduru, Njombe na Sumbawanga, miji
mingine ambayo itaona tukio hilo kwa ukaribu zaidi wa asilimia 96 ni
Katavi, Nachingwea na Songea ikifuatiwa na Kigoma, Iringa, Mtwara na
Lindi.
Akizungumza jana na waandishi habari za Utalii na Uwekezaji Tanzania
(Tajati) nyumbani kwake katika Kata ya Isisi, Mwagongo alisema tukio
hilo la kupatwa kwa jua nchini si mkosi, bali ni sawa na taa iliyokuwa
imezimika na sasa imewashwa na kuongeza kuwa, ni ishara kuwa Mungu
ameukubali utawala uliopo madarakani na ndiyo sababu ametoa giza na
kuleta nuru.
Aliwaasa viongozi wa dini zote kote nchini kuliombea tukio hilo ili
lifanyike na kupita kwa amani na pasiwepo na uvunjifu wa amani
utakaosababisha jamii kutoa tafsiri ya tofauti baada ya tukio hili la
kihistoria ambalo litafanyika kati ya saa 4.15 asubuhi hadi saa 8.00
mchana.
Alisema baada ya tukio hilo, wazee wa kimila watachinja ng’ombe kwa
ajili ya kumshukuru Mungu kwa neema ya tukio hilo na pia kumwomba
aiepushe jamii na madhara yoyote yanayoweza kujitokeza.
“Hapo zamani watoto walikuwa hawaruhusiwi kutoka nje siku ya tukio
hili. Wazee waliamini ni ajali ya kugongana jua na mwezi na wanaoumia ni
wanadamu hasa watoto kwa kusababishiwa milipuko ya magonjwa
mbalimbali,” alisema katibu huyo na kuongeza:
“Lakini kwa sasa tunatambua kuwa ni tukio la kisayansi na kutokea
kwenye eneo letu ni neema kutoka kwa Mungu. Kupitia tukio hili dunia
itaijua Tanzania, itaijua Mbarali na itaijua Rujewa. Ni tukio ambalo
limetutangaza.”
Kwa upande wa walimu na wanafunzi katika shule mbalimbali mjini
Rujewa walionesha kuwa na furaha kubwa ya ujio wa tukio hilo wakisema
watapata fursa nzuri ya kujifunza kwa vitendo kwa kuwa watajionea badala
ya kusimuliwa au kusoma kwenye vitabu.
Mwalimu wa taaluma katika Shule ya Msingi Isisi, Donatha Nkwera
alisema walimu shuleni hapo wamewaandaa wanafunzi kwa ajili ya tukio
hilo linalotokea jirani na shule yao.
Wakati hayo yakiendelea, baadhi ya huduma za kijamii zimeonekana kukosekana kutokana na wingi wa wageni waliofika wilayani hapa.
Moja ya huduma hizo ni nyumba za kulala wageni ambapo licha ya vyumba
kuwa vya shida pia baadhi ya wamiliki wa nyumba hizo wamepandisha bei
za kupanga kutoa Sh 10,000 hadi Sh 30,000.
Kadhalika, huduma muhimu zikiwemo za mawasiliano zilionekana kuwa za
shida hadi jana kutokana na umeme kukatika tangu saa mbili asubuhi hadi
jioni, hivyo kuleta usumbufu na kukwamisha baadhi ya kazi.
Thursday, 1 September 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment