.

.

Wednesday, 17 August 2016

YANGA na Azam leo zinakutana kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam katika mechi ya Ngao ya Jamii kuashiria uzinduzi wa Ligi Kuu inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi mwishoni mwa wiki hii.
Timu hizo kwa muda mrefu zimekuwa zikipokezana kijiti kwenye anga za soka la kitaifa na kimataifa ambapo mwaka huu.
Azam ilishiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na kutolewa mapema na Yanga iliyokuwa ikishiriki Ligi ya Mabingwa kabla ya kuangukia kwenye Kombe la Shirikisho ipo hatua ya makundi ya michuano hiyo licha ya kutokuwa na nafasi ya kusonga mbele.
Mara ya mwisho timu hizo zilikutana kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho la TFF katika Uwanja wa Taifa ambapo Yanga ilishinda mabao 3-1. Aidha Yanga iliendelea kuitambia Azam tena katika mechi ya ngao ya Jamii msimu uliopita ambapo iliichapa kwa mikwaju ya penalti 8-7 baada ya kutoka sare ya bila kufungana kwa dakika 120 .
Katika mechi ya leo, Yanga itashuka dimbani ikitoka kupata ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Mo Bejaia Jumamosi iliyopita baada ya kucheza mechi nne mfululizo kwenye michuano hiyo bila ushindi.
Lakini pia, ikiwa na rekodi ya kupoteza michezo kadhaa iliyopita ya michuano hiyo dhidi ya TP Mazembe 1-0, Medeama ugenini (3-1) na nyumbani (1-1), Mo Bejaia ugenini (1-0).
Yanga sasa inasubiri kukamilisha ratiba dhidi ya Mazembe katika mechi ya mwisho ya makundi baada ya kutokuwa na nafasi ya kufuzu nusu fainali ya michuano hiyo kutokana na ushindi wa mabao 3-2 wa Medeama dhidi ya Mazembe mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kocha Mkuu wa Yanga Hans Pluijm alisema jana kuwa wamesahau yaliyopita na matarajio yao ni kushinda mchezo wa leo ili kuwa na mwanzo mzuri wa maandalizi ya Ligi Kuu Tanzania bara wakiwa mabingwa watetezi.
“Hakuna timu yoyote inayotutisha na kila siku tumekuwa tukifanya mazoezi na kujiimarisha, lengo letu ni kuendeleza rekodi ya kushinda mataji,” alisema.
Huenda Yanga ikawakosa wachezaji wake muhimu kama kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ anayesumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu, mabeki Juma Abdul, Andrew Vincent ‘Dante’ wanaosumbuliwa na maumivu ya miguu, Kevin Yondani anayeumwa jicho na kiungo Obrey Chirwa anayeumwa goti.
Aidha, mchezo wa leo utakuwa ni mtihani mkubwa wa kwanza kwa Kocha Mkuu wa Azam Mhispania Zeben Hernandez ambaye aliahidi kurejesha imani ya mashabiki wa Azam FC kwani anatarajia kutumia mfumo wa pasi nyingi ambao unatumiwa na timu ya Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’ Barcelona.
Timu hiyo imefanya maandalizi ya muda mrefu na kucheza mechi kadhaa za kirafiki ikiwa ni sehemu ya maandalizi yao ya ligi. Ilicheza dhidi ya URA ya Uganda (1-1), dhidi ya Friends Rangers (2-1), Ashanti United (2-0), Mshikamano (1-0), Kombaini ya Wilaya ya Mjini (1-0), Taifa Jang’ombe (1-0), na sare mbili ilipocheza na JKT Ruvu (1-1) na Ruvu Shooting (1-1).
Akizungumzia mchezo huo Hernandez, aliweka wazi kuwa ana uhakika mkubwa wa kuifunga Yanga kwenye mchezo wa leo kwani tayari amepata kikosi chake cha kwanza baada ya michezo hiyo ya kirafiki.
“Siwezi kuzungumzia sana mechi ya Yanga kwa sababu naamini ya kuwa jitihada zangu na taaluma ninayowapa wachezaji wangu naamini itatoa matunda, lakini natambua ya kuwa Yanga ni timu ya zamani ipo na inacheza vizuri, kikubwa naamini nitashinda mchezo huo kulingana na kile ninachowapa wachezaji wangu,” alisema.
Azam FC huenda ikawakosa wachezaji wake Aggrey Morris na Paschal Wawa ambao ni majeruhi wa muda mrefu, ingawa wameshaanza mazoezi mepesi. Lakini pia, wanajivunia usajili wa beki mpya Bruce Kangwa anayetokea Highlanders ya Zimbabwe.

0 comments:

Post a Comment