RAIS John Magufuli ameutaka uongozi wa Mkoa wa Mwanza, kuhakikisha
kuwa watu waliopora mali za Chama cha Ushirika cha Nyanza (NCU),
wanapatikana na kuzirudisha mali hizo mara moja, huku akiitaja Kampuni
ya Simon Group yenye umiliki katika kampuni za UDA na mabasi ya haraka
Dar es Salaam (UDA-RT).
Amesema NCU kwa sasa inashindwa kujiendesha kutokana na watu wachache
kujitwalia mali za NCU kwa kuzinunua kwa bei ya hasara, kiasi cha
kuifanya NCU kutokuwa na uwezo wa kununua mazao ya wakulima.
“RC (mkuu wa mkoa) umezungumza kwamba katika miaka yote aliyepewa
alikuwa anunue kwa bilioni moja pointi amelipa milioni 30 tu na nasikia
ni Simon Group. Mimi ni msemakweli na wala sitaki kuzunguka sijui
nikasemee wapi,” alisema Rais Magufuli akiitaja kampuni hiyo
inayomilikiwa na mfanyabiashara Simon Kisena.
Rais Magufuli aliyasema hayo jana jijini hapa wakati akiwahutubia
maelfu ya wakazi wa Mwanza kwenye Viwanja vya Furahisha vilivyopo
Manispaa ya Ilemela.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella alimshukuru Rais Magufuli
licha ya kuwa na ratiba ngumu ya kikazi, lakini ameonesha mapenzi
makubwa kwa wakazi wa Mkoa wa Mwanza na kufanya ziara ya kikazi ya siku
mbili.
Alisema mkoa umeanza na juhudi ya kufufua zao la pamba sanjari na
kuanza kurudisha mali za NCU, ambazo ziliporwa na baadhi ya watu,
alimuomba Rais Magufuli kuisaidia Serikali ya Mkoa ili kuhakikisha watu
wote waliopora mali za NCU wanazirudisha kwa wakulima na wafikishwe
mahakamani.
Lakini Rais Magufuli katika hotuba yake, alisema NCU kwa sasa
inashindwa kujiendesha kutokana na watu wachache kujitwalia mali zake
kwa kuzinunua kwa bei ya hasara, kiasi cha kuifanya kutokuwa na uwezo wa
kununua mazao ya wakulima.
“Hata kama walichukua miaka 20 iliyopita, vyombo vya dola vichukue
hatua na mali hizo zirudishwe kwa umma. Waziri wa Ushirika, ni heri
ukose kula, mimi nitakuchagua kwenye viti maalumu, lakini mali za Nyanza
zirudi,” alisema Rais Magufuli.
Aliwataka mafisadi wakae chonjo kuwa tayari kufikishwa mahakamani kwa
sababu Bunge tayari limeishaipitisha sheria hiyo, ambayo itaanza
utekelezaji wake mara moja.
Alisema sheria hiyo itakuwa ni mkombozi wa Watanzania ambao hivi sasa
wamechoka na rushwa, ambapo alikiri kuwa kwa sasa rushwa ipo kila
mahali nchini.
“Nawashukuru sana wabunge (hasa wa CCM) kwa kupitisha sheria hiyo ya mafisadi,” alisema Rais Magufuli.
Kuhusu uvuvi haramu kwa kutumia zana zisizokubalika kisheria, Rais
Magufuli alishangaa kuona vyombo vilivyopewa jukumu la kudhibiti hali
hiyo vikizembea wakati uharamia huo ukiendelea.
“Kama kuna mtu alichoma makokoro ni mimi na samaki waliongezeka.
Wanapita kuna Polisi, Uhamiaji, TRA, lazima tulinde rasilimali yetu ili
Watanzania waweze kufaidika. Hizo zana zinapitishwa kwenye mipaka,
shikeni na hilo gari mtaifishe moja kwa moja kwa sababu hayapiti
angani,” alieleza.
Katika hotuba yake, Rais Magufuli alisisitiza kuwa uchaguzi umekwisha
na kwamba hakuna aliyeshinda wala kushindwa, bali Watanzania wote
wameshinda. Alisisitiza kuwa atatekeleza ahadi zote alizoahidi wakati wa
Uchaguzi Mkuu ikiwamo kulifanya Jiji la Mwanza kuwa jiji la biashara.
Akizungumzia hatua ambazo amekwishazichukua hadi sasa katika uongozi
wake, alisema amebana matumizi ya serikali kwa kufuta safari zisizo za
lazima nje ya nchi, kutumbua watumishi hewa, kutoa elimu bure, na mwezi
ujao ndege mbili mpya zitatua nchini kutoka Canada zinaponunuliwa.
Akizungumzia upanuzi wa barabara ya Airport, Rais Magufuli
aliyeongozana na mkewe, Janet, alimtaka Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Edwin
Ngonyani, Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Patrick Mfugale kuhakikisha kuwa
ujenzi wa barabara hiyo hadi Airport, badala ya kuishia Pasiansi,
inajengwa haraka iwezekanavyo.
“Upanuzi wa barabara hii usiishie Pasiansi, uende hadi Airport na iwe
ni barabara yenye njia nne ili kusudi watalii wanapofika hapa watambue
kuwa wameingia jijini Mwanza,” alisema na kuongeza kuwa serikali itatoa
fedha za upanuzi wa barabara hiyo hadi Airport na kuahidi kutoa kiasi
cha fedha kitakachohitajika ukamilishaji ujenzi wake.
Aidha, alikerwa na ukusanyaji duni wa mapato yanayokusanywa kutoka
kwenye vitega uchumi vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuwataka viongozi
wote wa chama kuhakikisha kuwa wanakusanya mapato halali yanayolingana
na vitega uchumi walivyo navyo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Ngonyani aliwashukuru wakazi wa Mwanza
kwa kazi kubwa waliyofanya ya kumchagua Dk Magufuli kuwa Rais wa
Tanzania.
Friday, 12 August 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment