.

.

Thursday, 6 August 2015



Ama kweli Mbeya City msimu huu imepania, kwani imetangaza kula sahani moja na Yanga katika maandalizi yao ya Ligi Kuu Tanzania Bara. Unajua ikoje? Uongozi wa timu hiyo umesema unajua Yanga na Azam zimejifua vilivyo kupitia Kagame, lakini hiyo haiwapi shida kwani nao watatumia wiki zilizosalia kufanya yao mapema ili wafunike katika ligi.
Uongozi huo umesema moja ya mikakati yao ni kucheza mechi kadhaa za kimataifa na klabu toka nje ya nchi za Zesco ya Zambia na Bata Bullets ya Malawi ambazo zitacheza pia na Yanga hivi karibuni jijini Mbeya.
Kabla ya kucheza mechi hizo za kirafiki za kimataifa, Mbeya City itaanza na Yanga, Agosti 18, jijini Mbeya ambako Wanajangwani wataweka kambi kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam.
Katibu Mkuu wa timu hiyo, Emmanuel Kimbe alisema wapo kwenye mazungumzo na timu hizo ambazo pia zitacheza mechi za kirafiki na Yanga na kwamba wana asilimia kubwa ya kufanikisha mpango huo.
“Tunajua changamoto ambazo tutakabiliana nazo kwa Yanga na Azam, katika ligi maana hizo zimepata muda wa kujipima uwezo kwenye Kagame ndio maana tunataka kujifua kupitia timu zenye uwezo,” alisema.
Kimbe alisema pia katika mechi hizo zitawasaidia kujua uwezo wa wachezaji wao na kutambua kombeneshani, hivyo wanajifanya mazoezi kuhakikisha kile wanachokitarajia kinatimia.

0 comments:

Post a Comment