.

.

Saturday, 2 January 2016

Pazia la Mapinduzi Cup linafunguliwa rasmi leo mchana kwa michezo miwili, mchezo wa kwanza utaanza majira ya mchana kati ya mabingwa wa ligi kuu Tanzania bara Yanga SC dhidi ya Mafunzo ya Zanzibar.
Mchezo wa pili utachezwa saa 2:15 usiku kati ya Azam FC dhidi ya Mtibwa Sugar michezo yote itafanyika kwenye uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar.
Kundi hili linajumuisha timu tatu kutoka Tanzania bara ambazo zote zinashiriki ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara na zinafanya vizuri kwenye ligi hiyo, timu hizo ni Azam FC, Yanga SC na Mtibwa Suga huku Mafunzo ya Zanzibar ikikamilisha idadi ya timu nne za kundi hilo.
Azam ndiyo vinara wa ligi kuu Tanzania bara wakiwa na pointi 35 wakifuatiwa na Yanga wenye pointi 33 katika nafasi ya pili wakati Mtibwa Sugar wao wakiwa nafasi ya nne kwa pointi zao 27 sawa na Simba lakini wekundu wa Msimbazi wakikaa nafasi ya tatu kwa tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa.
Mchezo unaopewa uzito wa juu ni mchezo wa usiku kati ya Azam FC vs Mtibwa Sugar kwasababu timu hizo zimekutana Jumatano iliyopita kwenye mchezo wa ligi uliopigwa kwenye uwanja wa Azam Complex na kuishuhudia Azam FC ikipata ushindi wa goli 1-0 kwa mbinde mbele ya Mtibwa mchezo uliokuwa mkali na wa kuvutia.
Msimu uliopita Mtibwa ilicheza fainali ya michuano hiyo dhidi ya Simba na kupoteza mchezo huo kwa mikwaju ya penati na Simba ikafanikiwa kutwaa taji hilo kwa mara nyingine tena.

0 comments:

Post a Comment