DURU la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara linaanza leo wakati timu 12
zikiwemo za Yanga na Simba kushuka kwenye viwanja tofauti kusaka pointi
tatu muhimu. Hata hivyo, Azam FC inayoshika nafasi ya pili katika
msimamo wa ligi hiyo, leo ilitakiwa kucheza na Prisons ya Mbeya,
haitashuka dimbani kwa sababu inashiriki mashindano ya timu nne nchini
Zambia.
Yanga wenyewe wako kileleni wakiwa na pointi 39 sawa na Azam FC,
lakini wanaongoza kwa uwiano wa tofauti ya magoli, leo watakuwa wageni
wa Coastal Union katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani
mjini Tanga.
Katika mchezo wa raundi ya awali, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao
2-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Yanga watataka kudhihirisha kuwa hawakubahatisha kuifunga Coastal katika
mchezo wa kwanza, huku Wagosi hao wa Kaya nao watataka kudhihirisha wao
sio wanyonge mbele ya mabingwa hao watetezi.
Vijana hao wa Jangwani wakishinda leo watakuwa wamejikusanyia pointi
42 na kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo na kuiacha Azam FC
ikibaki na pointi zake 39 katika nafasi ya pili.
Kwa upande wa Simba, wenyewe katika mchezo wa kwanza dhidi ya African
Sports uliochezwa Mkwakwani, iliibuka na ushindi kiduchi wa bao 1-0,
hivyo na leo itataka kuendeleza ubabe dhidi ya vijana hao wa Tanga.
Simba yenye pointi 33, inazihitaji sana pointi tatu kutoka kwa
African Sports ili angalau izidi kujisogeza katika nafasi ya tatu nyuma
ya Azam katika mbio hizo za ubingwa wa ligi hiyo.
Kwa sasa Simba inafundishwa na Mganda Jackson Mayanja aliyechukua
nafasi ya Muingereza Dylan Kerr aliyetimuliwa licha ya timu hiyo kuwa
katika nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi hiyo.
Mayanja alisema pamoja na ugumu wa mchezo huo, watajitahidi kuibuka
na ushindi ili kuendelea kuzifukuza Yanga na Azam FC zilizoko kileleni.
Coastal Union na African Sports ziko katika nafasi ya 14 na 15 baada ya
kucheza mechi 15 na kuambulia pointi tisa na 10 badala ya kuwa na pointi
45 kutoka katika mechi hizo 15 za duru la kwanza.
Mechi zingine leo ni JKT Ruvu watakuwa wenyeji wa Majina ya Songea,
huku Mtibwa Sugar wakiikaribisha Stand United, wakati Mwadui FC
itaikaribisha Toto African wakati Kagera Sugar watacheza na Mbeya City
na Mgambo JKT watakuwa wenyeji wa Ndanda FC.
Ligi hiyo itaendelea tena kesho kwa Mgambo kuikaribisha Ndanda FC
kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga. Kwa upande wa ufungaji mabao,
Amis Tambwe ndiye anayeongoza hadi duru la kwanza linapomalizika baada
ya kupachika mabao 13 huku Hamisi Kiiza wa Simba akifuatia kwa mabao 10.
Saturday, 30 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment