WIZARA ya Elimu, Sayansi Teknolojia na Ufundi imeeleza baadhi ya
vigezo vitakavyotumika kupanga ada elekezi katika shule binafsi, kuwa ni
pamoja na aina ya huduma zinazotolewa kwa wanafunzi, mishahara ya
walimu.
Akizungumza jana bungeni wakati akijibu maswali ya wabunge
waliojadili Hotuba ya Rais John Magufuli aliyotoa wakati kuzindua Bunge,
Waziri wa Elimu, Sayansi Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako
alisema kutokana na vigezo hivyo, ada elekezi hizo haziwezi kufanana.
Profesa Ndalichako aliwaambia wabunge kwamba tayari wanaye mtaalamu
mshauri anayefanya kazi hiyo, ambaye baada ya kukamilisha kazi,
watakubaliana kwa ajili ya kutoa ada elekezi zitakazotofautiana
kulingana na viwango vya shule.
Kwa mujibu wa Profesa Ndalichako, mambo mengine yanayoangaliwa katika
huduma zinazotolewa shuleni ni pamoja na chakula, aina ya miundombinu,
viburudisho na mishahara ya walimu. Profesa Ndalichako aliwahakikishia
wabunge kwamba wizara inafanyia kazi suala hilo.
Alisema suala hilo linahitaji kufanyiwa kazi kwa kina, kwa kuangalia
vizuri makundi ya shule. “Unaweza kukuta huduma ambazo zinapatikana
shuleni zinatofautiana sana. Kuna shule nyingine mpaka zina swimming
pool (maeneo ya kuogelea), zimejengwa kwa terazo na nyingine zimejengwa
kwa marumaru.
Sasa unapotoa ada elekezi lazima uzingatie kwamba mwanafunzi anasoma
katika aina gani ya shule. “Zipo shule nyingine za binafsi ambazo hazina
hata sakafu, kwa hiyo huwezi kuja na ada elekezi, ukasema tu kwamba ni
shilingi kadhaa, lazima mambo haya yote uyaangalie.
“Hata chakula wanachokula wanafunzi kinatofautiana, baadhi ya shule
wanapewa mpaka soseji, wanakula pilau na wengine wanakula ugali na
maharage kila siku,” alisema. Profesa Ndalichako alisisitiza kwamba
haiwezekani kuja na ada elekezi zinazofanana, kwa hiyo wizara yake
lazima iangalie jambo hilo kwa umakini mkubwa.
“Kuna baadhi ya shule zinawaonea sana walimu, zinawalipa kidogo na
nyingine zinawalipa vizuri. Nawaomba Watanzania tuwe na subira, wizara
yangu inalifanyia kazi, lakini si jambo linalohitaji kufanyiwa kazi kwa
haraka, tutakapokuwa tayari tutakuja kuwapa majibu,” alisema.
Saturday, 30 January 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment