WAANGALIZI kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wameelezea
kushangazwa na amani na utulivu uliokuwepo wakati wa kupiga kura.
Kiongozi wa Timu ya Waangalizi wa Uchaguzi Mkuu kutoka EAC, Moody Awori,
ambaye pia ni Makamu wa Rais mstaafu wa Kenya amemueleza hayo Rais
Jakaya Kikwete alipofika Ikulu jana mchana.
“Sisi kutoka Kenya tulishangaa, unakwenda kwenye kituo watu wako
kimya, tunakupongeza pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM),” alisema
Awori. Aliongeza kuwa, “Tunatarajia kuwa uongozi mpya unaoingia
madarakani, utafuata nyayo zako.”
Awori alimueleza Rais kuwa katika shughuli zao za uangalizi,
walitembelea vituo zaidi ya 12 kwa siku jijini Dar es Salaam na kote
hali ilikuwa shwari. Alieleza kuwa wamejifunza kitu kikubwa katika
uchaguzi huo.
Watanzania kwa jadi yao ni watu wa amani na utulivu, lakini pia kabla
ya uchaguzi, Rais Kikwete aliweka wazi kuwa Serikali yake ina wajibu wa
kulinda watu na mali zao na kuhakikisha watu wote wanashiriki katika
kupata haki yao ya kupiga kura kwa amani, uhuru na utulivu bila
kubughudhiwa na hilo ndiyo jambo kubwa na la msingi kwa Serikali yake.
Awali jana asubuhi, Rais Kikwete alihudhuria hafla ya kukabidhiwa
vyeti kwa washindi wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Rais mteule Dk John
Magufuli na Makamu wa Rais mteule, Mama Samia Suluhu Hassan.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama na Serikali
na viongozi wa waangalizi wa uchaguzi hapa nchini, viongozi wa dini na
watu mbalimbali. Baadaye Rais Kikwete aliongoza mapokezi ya Rais mteule
katika Ofisi ndogo za CCM Lumumba, ambako wanachama, mashabiki na
wapenzi wa CCM walifika kumpokea na kumsalimia mgombea wao, ambaye
ameibuka mshindi wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Saturday, 31 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment