WAKATI wakisubiri matokeo ya uchaguzi ya rais huku Tume ya Uchaguzi
ikitangaza kura za wagombea wabunge na uwakilishi katika majimbo ya
uchaguzi Zanzibar, Jeshi la Polisi limelazimika kuzima fujo na vurugu
kutoka kwa wafuasi wa CUF waliotanda mitaa ya Mji Mkongwe na barabara
kuu ya Darajani.
Vurugu zimezuka baada ya mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim
Seif Sharif Hamad kufanya tathmini na kutangaza matokeo ya ushindi wa
chama chake katika uchaguzi wa juzi kwa asilimia 52.87. Maalim Seif
alitoa tathmini hiyo mbele ya waandishi wa habari katika Ofisi Kuu ya
CUF Mtendeni mjini Unguja na kuitaka Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC)
kutangaza matokeo hayo.
Katika tathmini hiyo inaonesha kwamba mgombea wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), kwa tiketi ya urais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amepata
ushindi kwa asilimia 47.13. Maalim Seif alidai matokeo waliyonayo
yamekusanywa na mawakala waliopo katika vituo vya uchaguzi vilivyopo
Unguja na Pemba kwa kufanya majumuisho. Hatua hiyo ilizusha shangwe na
furaha kwa wafuasi wa CUF na kuanza kutembea barabarani huku gari
zikipiga honi.
Baadhi ya mitaa ikiwemo Darajani na Mlandege, polisi waliweka vizuizi
ambavyo vilisaidia kuwazuia wafuasi hao kuingia barabarani. Aidha,
ofisi za Serikali zilizopo katika eneo la Mji Mkongwe pamoja na taasisi
za kibenki, zilifungwa baada ya kuibuka kwa mazingira ya fujo na vurugu.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Mkadam Khamis
Mkadam alithibitisha Jeshi la Polisi kudhibiti maeneo mbalimbali zaidi
yaliyopo Mji Mkongwe pamoja na eneo la Darajani ambalo ni ngome ya
upinzani.
“Tumefanikiwa kudhibiti vurugu za watu waliofanya fujo na vurugu
katika maeneo mbali mbali ya mji wa Unguja na hali ni shwari kwa sasa,”
alisema Mkadam. Kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar ni kosa la jinai kwa mtu yeyote au mgombea wa chama cha siasa
kutangaza matokeo ya urais. Mapema, CCM Zanzibar ililaani kitendo
kilichofanywa na Maalim Seif kujitangazia ushindi katika uchaguzi huo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM
Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema kitendo hicho ni sehemu ya vitendo na
matukio ya uchochezi yanayotakiwa kudhibitiwa kwa ajili ya kuimarisha
amani na utulivu. Vuai aliitaka ZEC kuchukua hatua za kisheria na
kinidhamu kwa mgombea huyo kwa kauli zake ambazo lengo lake kuingiza
nchi katika machafuko katika kipindi hiki kigumu cha uchaguzi.
Hata hivyo, viongozi watendaji wa ZEC hawakuwa tayari kulizungumzia
suala hilo, ambapo maofisa wote walikuwa wapo katika mchakato wa kupokea
na kutangaza matokeo ya uchaguzi wa majimbo.
Tuesday, 27 October 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment