.

.

Friday, 30 October 2015

DAKTARI wa Kemia, John Pombe Joseph Magufuli ndiye Rais wa Tano wa Tanzania.
Jana ambapo alitimiza miaka 56 ya kuzaliwa kwake, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilimtangaza kuwa mshindi wa Uchaguzi Mkuu wa Urais mwaka 2015, uliofanyika Jumapili iliyopita.
Mbunge huyo wa Chato kwa miaka 20, aliyezaliwa Oktoba 29, 1959, ametangazwa mshindi baada ya kupata kura 8,882,935, sawa na asilimia 58.46 ya kura halali zilizopigwa Jumapili, hivyo kumrithi Rais Jakaya Kikwete katika Ikulu ya Magogoni ambayo tayari imeshakaliwa na Watanzania wengine wanne.
Mbali ya Rais Kikwete, marais wengine waliowahi kuiongoza Tanzania ni Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa, ambao wameshika madaraka hayo ya juu ya nchi tangu Uhuru wa mwaka 1961.
Akitangaza matokeo hayo jana kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNCC), Dar es Salaam, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva alisema Dk Magufuli ameshinda nafasi hiyo baada ya kujikusanyia kura 8,882,935 ambayo sawa na asilimia 58.46 ya kura halali zilizopigwa.
“Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 Ibara ya 41 (6) mgombea yeyote wa kiti cha urais atatangazwa kuwa amechaguliwa kuwa rais, iwapo tu amepata kura nyingi zaidi kuliko mgombea mwingine yeyote. Na Ibara ya 47 (ii) inasema mgombea urais akichaguliwa kuwa mshindi, basi mgombea mwenza atatangazwa kuwa Makamu wa Rais,” alisema Jaji Lubuva.
“Kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi Kifungu wa 35 (e) na 35 (f) na Kifungu cha 81 (b) vya Sheria ya Uchaguzi Sura ya 343, namtangaza John Magufuli kuwa mshindi wa uchaguzi wa Rais wa mwaka 2015 na pia namtangaza Samia Suluhu Hassan kuwa Makamu wa Rais.” Kwa msingi huo, Mgombea Mwenza wa CCM, Samia Suluhu Hassan atakuwa Makamu wa Rais, akiwa ni mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo Tanzania tangu nchi ilipoundwa.
Dk Magufuli alifuatiwa na mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliyeungwa mkono na vyama vinne vya upinzani (Ukawa), Edward Lowassa aliyepata kura 6,072,848, sawa na asilimia 39.97 ya kura halali zilizopigwa.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kailima Kombwey, katika uchaguzi wa mwaka huu, wapiga kura 23,161,440 walijiandikisha na waliopiga kura ni 15,589,639, ambayo ni asilimia 67.31 ya waliojiandikisha.
Kombwey alisema kura halali ni 15,193,862 ambayo ni asilimia 97.46 na kura zilizokataliwa ni 402,248 ambayo ni asilimia 2.58. Katika uchaguzi huo, ambao wagombea wa urais walikuwa wanane, mwanamke pekee, Anna Mgwhira wa chama kipya cha ACT-Wazalendo alishika nafasi ya tatu kwa kupata kura 98,763 sawa na asilimia 0.65.
Wagombea wengine kura walizopata na asilimia kwenye mabano ni Chief Lutalosa Yemba wa ADC kura 66,049 (asilimia 0.43), Hashim Rungwe wa Chaumma kura 49,256 (asilimia 0.32), Janken Kasambala wa NRA kura 8,028 (asilimia 0.05), Macmillan Lyimo wa TLP kura 8,198 (asilimia 0.05), Fahmi Dovutwa wa UPDP kura 7,785 (0.05%).
Katika uchaguzi uliofanyika mwaka 2010, mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete alishinda uchaguzi huo akiwa amepata asilimia 61.17 baada ya kupata kura zaidi ya milioni 5.27 na kufuatiwa na mgombea wa Chadema, Dk Willbrod Slaa aliyepata kura ya zaidi ya milioni 2.27.
Nafasi ya tatu ilikwenda kwa Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF aliyepata kura 697,014, Peter Mziray alipata kura 96,932, Rungwe aliyegombea kwa tiketi ya NCCRMageuzi alipata kura 26,321, Mutamwega Mughwaya wa TLP alipata kura 17,434 na Dovutwa alipata kura 13,123. Ujumlishwaji wa matokeo ulishuhudiwa na mawakala wa vyama mbalimbali, waangalizi, Polisi pamoja na wananchi wa kawaida, pamoja na kuhakiki matokeo hayo.
Hata hivyo, vyama viwili kati ya vinane vilivyoshiriki uchaguzi havikusaini matokeo hayo ambavyo ni Chadema na Chaumma. Chadema katika majumuisho, wakala wake Goodluck ole Medeye, waziri wa zamani katika Serikali ya Awamu ya Nne aliyemfuata swahiba wake Lowassa katika Chadema, ambaye alikuwepo wakati wa kutangaza matokeo ya majimbo, hakuwepo wakati wa kujumuisha na kusaini matokeo huku wakala wa Chaumma akigoma kusaini.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Kailima Kombwey alisema pamoja na mawakala hao kugoma kusaini hakuzuii, Tume kutangaza matokeo ya uchaguzi. Kwa mujibu wa Kombwey, Rais mteule Dk Magufuli atakabidhiwa cheti cha ushindi leo kwenye Viwanja vya Diamond Jubilee, Dar es Salaam pamoja na Makamu wa Rais, Samia.
Dakika chache kabla ya Dk Magufuli kutangazwa na NEC baada ya kumaliza kujumuisha matokeo, ambayo yalianza kutangazwa kwa umma kuanzia Jumatatu asubuhi, Rais Kikwete aliweka picha ya Magufuli katika akaunti yake ya Twitter na kuandika, “Amiri Jeshi Mkuu mpya wa Tanzania, chaguo la Watanzania, Rais John Pombe Magufuli.”
Aidha, mgombea wa ACT – Wazalendo, Anna Mghwira alimpigia simu Dk Magufuli muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi na kumpongeza, huku Dk Magufuli akimshukuru na kumwita mkomavu wa siasa na mwanademokrasia wa mfano.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, baada ya kupiga kura kijijini kwake Msoga wilayani Bagamoyo, ataondoka madarakani kwa mujibu wa Katiba Alhamisi ya Novemba 5, mwaka huu, siku ambayo Dk Magufuli atakula kiapo kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kuiongoza Tanzania kwa miaka mitano ijayo.
Dk Magufuli ambaye ni Waziri wa Ujenzi, atakuwa Rais wa kwanza wa Tanzania ambaye ni mwanasayansi, na pia mwalimu wa tatu kukaa Ikulu ya Magogoni, akitanguliwa na walimu wenzake Mwalimu Nyerere na Alhaj Mwinyi.
Amewahi kufundisha katika Shule ya Sekondari ya Sengerema mkoani Mwanza akifundisha masomo ya Kemia na Hisabati, na baadaye kufanya kazi katika Chama cha Ushirika cha Nyanza jijini Mwanza akiwa Mkemia.
Alijitosa katika siasa ambako alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Mashariki mkoani Kagera (wakati huo sasa Chato mkoani Geita) mwaka 1995. Amekuwa mbunge wa jimbo hilo hadi Juni mwaka huu, alipojitosa katika mchakato wa kuwania urais. Aliteuliwa na Rais Mkapa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2005. Baadaye alikuwa Waziri kamili wa wizara hiyo.
Chini ya Rais Kikwete, amewahi kuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kabla ya kumrejesha Ujenzi. Dk Magufuli anasifika kwa uchapakazi na weledi katika kazi zote, alizokabidhiwa akiwa serikalini na wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu kaulimbiu yake ilikuwa “Hapa Kazi Tu”.
Kaulimbiu hiyo ilimbeba na kumpambanua na wagombea wengine saba, huku akiahidi kuwa Tanzania itakuwa nchi ya viwanda chini ya uongozi wake. Katika uchaguzi uliokuwa na ushindani mkubwa pengine kuliko chaguzi nyingine nne za mfumo wa vyama vingi ulioanzishwa mwaka 1992, Dk Magufuli aliendesha kampeni zake, akijipambanua kuwa ni mtu atakayeleta mabadiliko ya kweli katika utendaji wa serikali.
Aliwaahidi Watanzania kwamba atasimamia mabadiliko hayo katika kila sekta, akisisitiza zaidi maendeleo ya viwanda hasa katika kuiwezesha Tanzania kuingia kuwa nchi ya uchumi wa kati.
Akifunga kampeni zake jijini Mwanza kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Dk Magufuli alisema amepokea ushauri kutoka kwa wananchi kwa njia mbalimbali, kutoka facebook, tweeter, mabango, vikao mbalimbali na hata ujumbe mfupi wa simu ambapo alisema imeonekana kero kubwa ni maji.
Kero nyingine alizoahidi kushughulikia ni ya nishati ya umeme, kulinda Muungano, kuendeleza ulinzi na usalama wa nchi na wananchi wake, kuimarisha kilimo, uvuvi na ufugaji kwa kuboresha bei ya mazao ya kazi hizo na kuimarisha viwanda, viongeze thamani ya mazao hayo.
Aliahidi kuhakikisha kila Mtanzania mwenye uwezo wa kufanya kazi anapata kazi yenye kipato kizuri, kutoa mikopo ya Sh milioni 50 kila kijiji na mtaa ya kuanzisha na kuendeleza biashara, kuhakikisha elimu inatolewa bure kuanzia awali mpaka kidato cha nne na kuwashughulikia mafisadi kwa kuanzisha Mahakama ya Rushwa.
Mshindani wake wa karibu, Waziri Mkuu wa zamani, Lowassa ambaye alikuwa ndani ya CCM kabla ya kujitoa Agosti mwaka huu, aliingia Chadema na kubeba kaulimbiu ya mabadiliko, huku akiwaahidi Watanzania kuwa ataendesha serikali kwa mchakamchaka na kubadili hali ya maisha kwa Watanzania kwa muda mfupi.

0 comments:

Post a Comment