.

.

Friday, 30 October 2015

KOCHA wa Yanga Hans van der Pluijm, ameitupia lawama safu yake ya ulinzi kwa kusema ilikosa umakini na kusababisha wapinzani wao Mwadui FC kusawazisha bao la pili dakika za mwisho.
Yanga juzi ilikuwa ugenini Uwanja wa Kambarage Shinyanga kupambana na Mwadui FC, na kulazimishwa sare ya 2-2, matokeo ambayo yameiweka rehani nafasi yake ya kuongoza ligi hiyo.
Akizungumza na gazeti hili Pluijm, alisema safu yake ya ulinzi iliwanyima pointi tatu kwenye mchezo huo kitu ambacho kinaweza kuwagharimu kutokana na ushindani mkali uliopo kati yao na wapinzani wao Azam FC.
“Hatukucheza kwenye kiwango chetu cha kawaida, lakini tulistahili ushindi kutokana na namna ambavyo wachezaji wangu walivyocheza kwa kujitolea na kupata mabao yale mawili.
“Hata hivyo safu yetu ya ulinzi ilituangusha kwa kuruhusu bao la kusawazisha la dakika za mwisho,” alisema Pluijm. Mholanzi huyo alisema matokeo hayo siyo mabaya, lakini wanalazimika kupambana kwenye mchezo wao unaokuja dhidi ya Kagera Sugar ili kurudisha wimbi lao la ushindi na kuendelea kujiwekea mazingira mazuri ya ubingwa msimu huu.
Alisema katika mchezo huo wapinzani wao Mwadui, walionekana kucheza kwa kutumia nguvu nyingi na kuwakamia, kitu ambacho kiliwasumbua wachezaji wake kushindwa kuonesha kiwango chao cha kawaida ambacho wamekuwa wakikionesha kwenye michezo iliyopita.
“Mchezo ulikuwa mgumu kwa sababu tulicheza na timu ambayo ilipania kutuvurugia mipango yetu kwa kucheza vurugu, lakini nimefurahi kupata sare hiyo kwa sababu vijana wangu walilazimika kubadilika na kuendana na hali ya mchezo ilivyokuwa,” alisema Pluijm.
Katika mchezo huo mabao ya Yanga yote mawili yalifungwa na Mzimbabwe Donald Ngoma, huku yale ya Mwadui yakifungwa na Poul Nonga na Bakari Kigodeko na kuifanya timu hiyo ya Jangwani kufikisha pointi 20 katika mechi nane ilizocheza msimu huu.

0 comments:

Post a Comment