.

.

Sunday, 2 August 2015

AZAM FC jana iliweka historia kwa kutwaa kwa mara ya kwanza taji la Kagame baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Gor Mahia ya Kenya katika fainali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.
Ubingwa huo wa Azam FC umemaliza ubabe wa Yanga na Simba kwa Tanzania kutwaa taji hilo, ambalo limechukuliwa na wekundu wa Msimbazi mara sita huku vijana wa Jangwani wakilitwaa mara tano.
Mbali na kumaliza ubabe wa vigogo hivyo, Azam FC pia imeweka historia nyingine baada ya kumaliza mashindano hayo bila ya kufungwa bao hata moja kuanzia mwanzo wa mashindano hayo hadi mwisho.
Pia, Azam imemaliza ukame wa taji hilo ililonusurika kulitwaa mwaka 2012 ilipofungwa na Yanga 2-0 katika fainali iliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa. Katika mchezo huo, Azam FC ndio walikuwa wa kwanza kulifikia lango la Gor Mahia mara mbili mwanzoni kabisa mwa mchezo, kabla wapinzani wao hawajajibu wakati Medieval Kagere alipotaka kufunga.
Dakika ya 15 John Bocco aliipatia Azam bao la kwanza akimalizia krosi ya Kipre Tchetche. Muda mfupi kabla ya mapumziko, Azam FC ilionekana kupungukia nguvu na kuifanya Gor Mahia kufanya mashambulizi ya mara kwa mara katika lango la wapinzani wake hao.
Dakika ya 51 Azam nusura wapige bao la pili baada ya Tchetche kupiga shuti kali lililogonga mwamba wa pembeni na mpira kurudi uwanjani kabla haojaokolewa. Juhudi za Azam zilizaa matunda wakati Tchetche alipoipatia timu yake bao la pili baada ya kupiga mpira wa adhabu uliokwenda moja kwa moja wavuni ukimuacha kipa wa Gor Mahia Boniface Oluoch akidua bila la kufanya.
Mwamuzi alitoa adhabu hiyo baada ya Shomari Kapombe kuchezewa rafu na Aucho Khalid aliyeoneshwa kadi ya njano kwa mchezo huo mbaya. Azam FC wangeweza kufunga la tatu kama sio kukosa umakini kwa mchezaji wake, Didier Kavumbagu baada ya kukosa bao la wazi katika dakika ya 90 wakati alipopaisha mpira.
Vikosi: Azam FC: Aishi Manula, John Bocco, Aggrey Morris, Said Morad, Pascal Wawa, Jean Mugiraneza, Humid Mao, Farid Mussa/ Erasto Nyoni, Amme Ali/Frank Domayo, Shomari Kapombe na Kipre Tchetche. Gor Mahia: Boniface Oluoch, Mussa Mohamed, Sibomana Abouba, Harun Shakava, Karim Nizigayamana, Innocent Wafula, Such Khalid, Godfrey Walusimbi, Kagere Medie, Michael Olunga na Erick Ochieng.

0 comments:

Post a Comment