Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye
MAKADA wa CCM waliotangaza nia ya kuwania urais, sasa wamefikia tisa
baada ya jana Profesa Sospeter Muhongo, Frederick Sumaye na Dk Titus
Kamani, kutangaza rasmi dhamira hiyo wakiwa katika miji mitatu tofauti
nchini.
Sumaye, Waziri Mkuu mstaafu alitangaza nia akiwa Dar es Salaam,
Profesa Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini aliyejiuzulu hivi karibuni
alitangaza akiwa Musoma wakati Dk.
Kamani ambaye ni Waziri wa Maendeleo na Mifugo na Uvuvi alitangaza nia akiwa Mwanza.
Wengine waliokwishatangaza ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa,
Waziri wa Kilimo, Chakula la Ushirika, Stephen Wassira, Naibu Waziri wa
Fedha, Mwigulu Nchemba, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu)
Profesa Mark Mwandosya, Mbunge wa Afrika Mashariki, Charles Makongoro
Nyerere na Balozi mstaafu, Ali Karume.
Sumaye na rushwa, ufisadi Sumaye, akitangaza rasmi nia yake jijini
Dar es Salaam, alisema endapo atapatiwa ridhaa na chama chake pamoja na
Watanzania atapambana kwa hali na mali kuondoa tatizo la rushwa na
ufisadi.
Sumaye aliyeshika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwa ni pamoja na
uwaziri mkuu kwa miaka 10, alisisitiza kuwa ametangaza nia hiyo kwa kuwa
tayari ameshapima, ametafakari na kujiridhisha kuwa anatosha kuwaongoza
Watanzania.
“Mimi naweka wazi leo hii, tatizo la ufisadi na rushwa kwangu
halivumiliki kwanza nayachukia kabisa matendo hayo. Nawahakikishia
Watanzania mkinipa ridhaa nipatambana na rushwa na ufisadi kwa ujasiri
bila uoga wowote, nitawashughulikia wote watakaohusika bila kujali sura,
vyeo, urafiki wala nafasi zao katika nchi hii,” alisisitiza.
Alisema amewasikia baadhi ya wagombea wenzake wa nafasi ya urais
ndani ya CCM, kila mmoja kwa wakati wake akizungumzia kupambana na
rushwa.
Aliongeza kuwa “Kuna mmoja wao anasema eti Watanzania hawataki
kiongozi masikini kwa hiyo huyu kwa namna nyingine anataka kiongozi
tajiri, cha kushangaza mtu huyo anasema yeye si tajiri bado anatafuta
utajiri, tena anataka urais, sasa swali hivi Ikulu ndiko kwenye
utajiri?” Alihoji Sumaye.
Akizungumzia sababu za kutaka kuwania urais, Sumaye aliyejaribu urais
mwaka 2010, alisema pamoja na kujipima na kuona anatosha, Watanzania
wengi wanamtambua kutokana na kuwa kiongozi wa muda mrefu ambaye
alitumikia Serikali ya awamu ya tatu kwa uadilifu na mafanikio makubwa.
“Tangu mwaka 1985 nimekuwa mbunge, nimekuwa Naibu Waziri, nikawa
Waziri, na baadaye Waziri Mkuu kwa miaka 10 mfululizo, kwa hiyo kama ni
jeshini mimi ni yule unayeweza kusema mwanajeshi aliyeiva na si
kuchupia,” alisisitiza.
Akizungumzia suala la ubinafsishaji wa mashirika ya umma na uuzwaji
wa nyumba za Serikali, Sumaye alisema Serikali yake ilitekeleza mipango
hiyo kutokana na Sera iliyokuwepo ambayo ilipitiwa na kujadiliwa na
Baraza la Mawaziri na Rais kushauriwa.
Aidha, alizungumzia kashfa za benki ya NBC, Rada, Mgodi wa Kiwira,
ndege ya Rais zilizoikumba Serikali yake na kubainisha kuwa katika
maeneo yote tajwa, hakuna hata moja lenye sifa ya kashfa kwa kuwa
yalibinafsishwa kwa taratibu zilizotakiwa huku mengine yakiwa na hali
mbaya.
“Tena Kiwira ndio ilikuwa na hali mbaya tangu zamani, bahati mbaya tu
akina Daniel Yona na Rais Benjamin Mkapa waliwekeza, kutokana na hali
yake Rais Mkapa alijitoa baada ya siku tatu tu,” alisema.
Alisema endapo atapewa ridhaa na chama chake na Watanzania,
vipaumbele vyake vitakuwa ni uchumi, rushwa, huduma za jamii, muungano,
umoja na amani. Katika rushwa ataunda Mahakama maalumu ya kusimamia na
kushughulikia kesi za rushwa na ufisadi.
Sumaye alisisitiza kuwa endapo chama hicho kitateua mgombea
anayependa rushwa au fisadi, msimamo wake ni kujitoa kwenye chama hicho.
“Ila sijajiandaa kujitoa, kwa kuwa najua chama changu chenye viongozi
wengi makini, hakitoweza kamwe kuteua mgombea mwenye sifa mbaya ya
ufisadi na rushwa,” alisema.
Muhongo na uchumi Profesa Muhongo amewaomba wana CCM na Watanzania
ridhaa ya kugombea urais Oktoba, akisema ana uwezo wa kupaisha uchumi
kwa kutumia rasilimali zilizopo, hivyo kumaliza umasikini.
Aliomba ridhaa hiyo jana katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT)
wilayani Musoma mkoani Mara, na kueleza kuwa atatenga bajeti ya kutosha
kwa ajili ya utafiti, ili ukuzaji uchumi na ushindani usifanywe kwa
kubahatisha.
Katika maelezo aliyoyatoa kuanzia saa 10:00 jioni, Muhongo alisema
kupitia mapinduzi atakayoyafanya katika sekta za elimu, viwanda, kilimo,
ufugaji, uvuvi, gesi na madini, kwa kuzingatia utafiti zaidi,
atasababisha kukua kwa ajira na pato la taifa, kufikia zaidi ya Dola za
Marekani bilioni 200, baada ya miaka 10 kuanzia atakapokuwa Rais.
Muhongo aliyekataa kuahidi chochote kuhusu mishahara ya watumishi wa
umma, na ujenzi wa shule, hadi aimarishe uchumi kwa kuiacha nchi ya
Kenya mbali, alisema; “Nitahakikisha gesi tuliyonayo inatuletea manufaa
katika viwanda na kuianzishia mfuko maalumu ili fedha zake zisiende
Hazina, kutoa fursa kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wazalishaji
wengine nchini, kukopeshwa mitaji kwa asilimia mbili”.
Mbali na vipaumbele vya utafiti na mapinduzi katika sekta ya gesi,
Profesa Muhongo alitaja vingine kuwa ni elimu, aliyoeleza kwamba
ataiongezea bajeti na kuboresha maslahi ya walimu na kuwalipa mishahara
sawa na madaktari, kama wafanyavyo Finland, kuongeza vifaa vya elimu na
kupunguza idadi ya wanafunzi darasani kuwa kati ya 15-35.
Akitoa ufafanuzi wa jinsi atakavyotekeleza vipaumbele vyake na kukuza
uchumi, Professa Muhongo alisema, atatumia utaalamu na wataalamu
waliopo na atakao waongeza kuhakikisha gesi inaleta mtaji wa Sh bilioni
500 na kuchangia kuzalisha umeme mwingi zaidi.
“Tumegundua gesi kiasi cha futi za ujazo trilioni 56, sawa na mapipa
bilioni 10 ya mafuta, yanayoweza kutuletea fedha hizo, hivyo kutuweka
katika nafasi nzuri ya kukuza uchumi wa nchi,” alisema.
Kamani na rasilimali za nchi Dk Kamani aliainisha vipaumbele sita
muhimu, alivyodhamiria kuvitekeleza katika Serikali yake, endapo
atafanikiwa kuingia madarakani, akisema atajikita katika kuimarisha
mshikamano wa uongozi unaoshirikisha wananchi katika matumizi ya
rasilimali za taifa.
Vipaumbele vyake vingine ni uadilifu kwa taifa, ili kuwawezesha
viongozi wa ngazi zote kufanya kazi kwa uadilifu, elimu kwa wote, kuweka
mazingira bora ya ajira serikalini na katika sekta binafsi, kuimarisha
huduma za afya kwa wananchi wote bila ya kubagua dini, kabila wala rangi
zao na kuhakikisha kuwa rasilimali ya nishati, inawanufaisha watu wote
na kuhakikisha nchi inakuwa na miundombinu imara muda wote.
Alisema katika uongozi wake, atadhamiria kuijenga Tanzania moja,
yenye upendo, amani na mshikamano, uadilifu lakini yenye kuwajali watu
wake bila ya kubagua, huku wakiwa na urari sawia wa kumiliki rasilimali
za nchi.
Katika kuwa na uhakika wa rasilimali fedha, alisema serikali yake
itajiweka mazingira mazuri ya ukusanyaji wa maduhuri ya serikali kwa
kuangalia upya vipaumbele vya ujenzi wa uchumi wa taifa, huku akiapa
kushughulikia wazembe na wala rushwa.
“Bila ya kudhibiti rushwa taifa litaangamia, nitakuwa mkali katika swala la rushwa”, alisema.
Imeandikwa na Halima Mlacha na Namsembaeli Mduma (Dar), Nashon Kennedy (Mwanza) na Ahmed Makongo (Musoma).
Wednesday, 3 June 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment