Simba na Singano wamekuwa kwenye mgogoro kwa takriban wiki ya pili sasa, ambapo mchezaji huyo anadai kutaka kuondoka kwa vile amemaliza mkataba wake wa miaka miwili huku uongozi wa klabu yake ukisema bado mchezaji wake halali kwani alisaini mkataba wa miaka mitatu unaotarajiwa kumalizika mwakani.
Taarifa ya TFF kwa vyombo vya habari jana ilisema imepokea kwa masikitiko taarifa za mgogoro wa kimkataba kati ya Singano na Simba.
“TFF imeagiza mwakilishi wa klabu ya Simba pamoja na mchezaji wa Simba wafike ofisi za TFF siku ya Jumanne tarehe 09/06/2015 kwa mazungumzo,” ilisomeka taarifa hiyo.
Aidha taarifa hiyo ilisema kila upande unatakiwa kufika na vielelezo vyake.
“Katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye mazungumzo, TFF inaziasa pande zote mbili zijiepushe na kutoa matamko yanayoweza kuchochea hali ya kutoelewana na kuamsha hisia mbaya katika familia ya mpira wa Miguu Tanzania,” ilisomeka taraifa hiyo.
Mwanzoni mwa wiki hii Simba ilitishia kumshitaki mchezaji huyo, kwa madai ameidhalilisha klabu kwa kitendo chake cha kudai hajasaini mkataba wa miaka mitatu na kumtaka apeleke mkataba wake wa miaka miwili anaodai alisaini.
Katika moja ya malalamiko yake, Singano ambaye anahusishwa na kutaka kujiunga na Azam anasema uwepo wake Simba haujamnufaisha kwani licha ya kufanya vizuri lakini hana pakuishi mpaka sasa.
0 comments:
Post a Comment