Waziri wa zamani wa Fedha, Basil MrambHUKUMU ya kesi ya kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 11.7
inayowakabili Waziri wa zamani wa Fedha, Basil Mramba, Waziri wa zamani
wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha,
Gray Mgonja inatarajiwa kutolewa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu.
Jopo la mahakimu watatu, John Utamwa, Sam Rumanyika na Saul Kinemela,
linatarajia kutoa hukumu hiyo baada ya kupitia ushahidi pamoja na
vielelezo vilivyowasilishwa na pande zote mbili katika kesi hiyo.
Katika kesi hiyo washitakiwa walikuwa wanakabiliwa na mashitaka
mawili ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara
ya Sh bilioni 11.7.
Upande wa Jamhuri uliita mashahidi saba na mahakama iliwaona
washitakiwa wana kesi ya kujibu, na katika utetezi wao washitakiwa
walijitetea wenyewe na kuita mashahidi wawili. Baada ya upande wa
utetezi kufunga ushahidi wao, mahakama imetoa nafasi kwa pande zote
mbili kuwasilisha hoja za kuishawishi kuwaona washitakiwa hao wana hatia
au hawana hatia.
Kwa mara ya kwanza washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo mwaka
2008 ikiwa ni miaka sita iliyopita, wakikabiliwa na mashitaka ya
kuisababishia serikali hasara ya kiasi hicho cha fedha kutokana na kutoa
msamaha wa kodi kwa Kampuni ya kukagua madini ya dhahabu ya M/S Alex
Stewart ya Uingereza.
Katika utetezi wake, Mramba alikiri kuisamehe kodi kampuni hiyo kwa
kuwa kulikuwa na mkataba uliosainiwa Juni 2003 kati ya kampuni hiyo na
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambao ulikuwa unaonesha malipo yafanyike
bila ya kukatwa kodi.
Mgonja alidai kuwa yeye ndiye aliyemshauri Mramba kuisamehe kodi
kampuni hiyo kutokana na mkataba huo. Hata hivyo, inadaiwa msamaha wa
kodi ulitolewa wakati tayari Wizara ilikuwa imepokea barua za kutoka
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambazo zilikuwa zinakataza kampuni hiyo
isisamehewe kodi.
Wakati huo huo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jana imeshindwa
kutoa hukumu ya kesi ya wizi wa Sh mlioni 207 kutoka katika akaunti ya
Madeni ya Nje (EPA) iliyopo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inayomkabili
Kada wa CCM, Rajabu Maranda na wenzake wanne kwa kuwa mshitakiwa mmoja
amelazwa.
Jopo la Mahakimu watatu linaloongozwa na Hakimu Mkazi, John Utamwa,
Ignas Kitusi na Eva Nkya liliahirisha hukumu hiyo hadi Julai Mosi mwaka
huu baada ya kuelezwa kuwa, aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Madeni ya Nje (
EPA), Iman Mwakosya amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
Kitengo cha Watu wenye matatizo ya akili.
Kabla ya kuahirisha kesi hiyo, mahakama imesema itaandika barua
kupeleka katika Hospitali Muhimbili, wafahamu hali ya kiakili aliyonayo
Mwakosya kama ataweza kuelewa mwenendo wa mahakama , ili waweze kusoma
hukumu hiyo.
Mbali na Maranda na Mwakosya washitakiwa wengine wanaokabiliwa na
kesi hiyo ni Farijala Hussein ambaye anatumikia kifungo cha miaka mitatu
jela, aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa EPA, Ester Komu na aliyekuwa Katibu
wa BoT, Bosco Kimela.
Wanakabiliwa na kesi ya wizi wa Sh milioni 207 kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) iliyopo Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Washitakiwa hao wanadaiwa kuwasilisha nyaraka za uongo, kughushi na
kuiba zaidi ya Sh milioni 207 kutoka BoT, aidha wanadaiwa kughushi
nyaraka ikiwamo hati ya makubaliano ya kuhamisha deni kutoka kampuni ya
General Marketing ya India kwenda kampuni ya Rashaz (T) ya Tanzania na
kuiba fedha hizo .
Tuesday, 30 June 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment