Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid jana aliwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya wizara yake kwa mwaka 2015/16, akiomba kuidhinishiwa Sh813 bilioni.
Kati ya fedha hizo, Sh444.6 bilioni kwa ajili ya
miradi ya maendeleo na Sh369.3 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
Kimsingi afya ni sekta mojawapo yenye changamoto lukuki hapa nchini. Ni
sekta muhimu katika kuchangia ustawi wa Taifa. Kumekuwa na changamoto
kadhaa katika sekta ya Afya. Hata hivyo Serikali imefanya jitihada
kubwa kukabiliana na changamoto hizo.
Baadhi ya jitihada hizo ni kupandisha viwango
vya hospitali, kukarabati na kuongeza majengo, kuongezeka kwa wataalamu
wa afya pamoja na huduma za kitaaluma katika baadhi ya hospitali zetu.
Lakini pamoja na jitihada hizo mabadiliko hayo
yamekuwa hayalingani na ongezeko la idadi ya watu pamoja na sayansi na
teknolojia. Kwa mfano tatizo la uhaba wa dawa limeendelea kuvikumba
vituo vyote vya Serikali hapa Tanzania kiasi cha kuwa chanzo cha vifo
vingi ambavyo vinatibika.
Tatizo jingine katika sekta hiyo ni upungufu wa
vifaa tiba. Vituo vingi vya tiba vimekabiliwa na upungufu huo na
kusababisha wagonjwa kutopata tiba kwa ufasaha hivyo kuhatarishaafya zao. Si ajabu hospitali kukaa muda mrefu bila kipimo cha wingi wa damu, kipimo cha sukari na hata X-Ray.
Uhaba wa dawa umekuwa ni tatizo kubwa nchini na
malalamiko mengi yametolewa. Kwa mfano mapitio ya kumbukumbu za Bunge ya
2008/09-2012/13 yanaonyesha takribani asilimia 35 ya wabunge ambao
huchangia katika mjadala wa bajeti ya afya, hulalamika uhaba wa dawa
vituoni na kuitaka Serikali kuongeza fedha.
Pia kuna tafiti kadhaa zimefanywa kuhusu tatizo la
uhaba wa dawa kwenye hospitali na vituo vya afya. Kwa mfano utafiti
uliofanywa na Taasisi ya Ifakara nchini (IHI), ulibaini kuwa katika
kipindi cha mwaka 2012 dawa muhimu zilizokuwepo katika vituo zilikuwa
asilimia 41 tu.
Kwa mujibu wa utafiti huo, hali hiyo ilimaanisha
kuwa kwa takribani asilimia 60 ya dawa muhimu hazikuweza kupatikana
katika vituo vya huduma za afya. Katika utafiti huohuo, ilibainika kuwa
dawa za antibiotics zilipatikanna kwa asilimia 57 tu, kitu ambacho ni hatari sana kwa magonjwa ya milipuko ambayo yamekuwa yakisababisha vifo.
0 comments:
Post a Comment