Aisha (katikati nyuma) akiwa na wanae watatu shuleni “TANGU nilipozaliwa mkoani Morogoro mwaka 1990, sikupata nafasi ya
kujiunga na masomo maana familia yetu ilikuwa ya kuhama hama na baba
hakuonesha nia ya kunisomesha kabisa.”
Ndivyo anavyoanza kusema Aisha Ally (25), mama mwenye mume na watoto
watatu ambao anasoma nao katika Shule ya Msingi ya Meru, jijini hapa.
Mama huyo anasoma darasa la tano huku mwanawe Philomena (9) akisoma
darasa la nne, Giftgod (5) akiwa darasa la kwanza pamoja na Thecla (3)
ambaye yuko shule ya awali hapo hapo katika Shule ya Msingi Meru.
Kisa, huruma Aisha aliyezungumza na gazeti hili wiki hii, amesema
matatizo yaliyoikumba familia yao huko nyuma, yalichangia ashindwe
kabisa kuhudhuria masomo na badala yake akajikuta akiolewa na kupata
watoto.
Kwa mujibu wa Aisha, alipanga kuanza darasa la kwanza kabisa, lakini
walimu wa Shule ya Msingi Meru walimshauri aanzie darasa la nne kwani
umri wake ulikuwa mkubwa.
Sababu nyingine iliyosukuma walimu watoe ushauri huo kwa mujibu wa
Aisha, ni binti yake mkubwa, Philomena ambaye wakati huo alikuwa darasa
la tatu na hivyo kama angeanza darasa la kwanza, angekuwa amemzidi mama
yake kwa darasa moja.
Viboko
Akizungumza kwa kujiamini, Aisha alisema umbo lake dogo na ufupi wa
kimo, vimemsaidia kuonekana kama mwanafunzi wa kawaida kiasi kwamba
baadhi ya walimu wasiojua historia yake na wageni, humchukulia kama
wanafunzi wengine tu na kumchapa viboko pale anapokosea.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Meru, Mussa Luambo amesema kuna
utaratibu maalumu wa kusaidia wanafunzi waishio kwenye mazingira magumu,
wakiwemo wale waliokosa elimu utotoni.
Kwa mujibu wa Mwalimu Luambo, Aisha ni miongoni mwa wanafunzi 20
walio kwenye kitengo hicho na baadhi ya walimu wameamua kuchangia fedha
kutoka mifukoni mwao ili kuwasaidia.
“Kwa kweli wanafunzi wenye umri mkubwa huwa hatuwachapi kabisa ila tu
kwa upande wa Aisha mwili wake mdogo huwa unamponza. Kuna walimu
wasiomfahamu hivyo hudhani ni mwanafunzi wa kawaida,” alisema Mwalimu
Luambo.
Mtoto ashuhudia
Akizungumza na gazeti hili, binti mkubwa wa Aisha, Philomena alisema;
“Wakati mwingine huwa tunachapwa viboko pamoja na maumivu yakizidi mimi
na wanafunzi wengine hulia machozi, lakini mama huwa halii kama sisi,
tena haogopi wala haoneshi kujali kupewa adhabu.”
Hata hivyo, Aisha anakiri kuwa viboko ndio suala linalomkera zaidi
shuleni hapo, kwani akishachapwa fimbo kadhaa za mkononi, baadae inakuwa
vigumu kwake kufanya kazi za nyumbani za kufua, kuosha vyombo na
kupika.
Biashara
Hivi karibuni alilazimika kuhamisha makazi yake na watoto kutoka eneo
la Moshono, alikokuwa akiishi na mumewe Shani Malepu na kuanza kuishi
katika chumba cha uani kwenye jengo ambalo amefungua biashara yake ya
duka mjini Arusha.
“Kule Moshono ni mbali sana na shule na ilikuwa inatugharimu nauli za
kila siku ili kuwahi masomo na mara nyingi tulikuwa tunachelewa kufika
shuleni,” alielezea Aisha. Mama huyo ana matarajio ya kuendelea na elimu
ya sekondari na anasema kuwa Mungu akimsaidia basi angependa kufika
hadi chuo kikuu kabisa.
“Mimi binafsi nina juhudi katika elimu, maana nilianza shule nikiwa
tayari najua kusoma maana nilikuwa najifunza mwenyewe nyumbani huku
nikiendelea na biashara zangu kama kawaida,” anasema.
Mume
Akizungumza na gazeti hili, mume wa Aisha, Malepu alisema haoni
tatizo kwa mama wa watoto wake kusoma shule ya msingi na wanawe. “Ni
uamuzi wake mwenyewe na anaonesha kupenda shule.
Tuliwahi kupanga kuwa ajiunge na vyuo vya ufundi stadi, lakini
baadaye akaona ni vyema zaidi ajiunge na elimu ya msingi na ninadhani
ana mpango wa kuwa mwalimu baadaye,” alisema.
Saturday, 6 June 2015
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment