Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni
Mchome amewataka Watumishi wa Wizara hiyo kuwa wabunifu zaidi na
kuhakikisha kuwa wanachokibuni kiwe kinatekelezwa na kuchukua hatua kwa
wasiotekeleza maelekezo ya kisera pamoja na kuwazawadia wanaotekeleza
kwa ufanisi maelekezo yanayotolewa.
“Watumishi wa Wizara hii tunatakiwa tujiulize tunafanya ubunifu gani ili
kuhakisha wahitimu katika ngazi mbalimbali wanapata maarifa
yanayotakiwa na wanaoweza kusaidia nchi katika kuleta maendeleo katika
nyanja mbalimbali,” alisema Profesa Mchome.
Profesa Mchome alikuwa akizungumza na Watumishi wa Makao Makuu na
Taasisi zilizoko chini ya Wizara hiyo katika Ukumbi wa Mikutano wa
Kimataifa wa Julius Nyerere (Julius Nyerere International Convention
Centre), Ijumaa 18 Julai, 2014 ikiwa ni utaratibu aliojiwekea wa
kukutana na watumishi hao na kujadiliana namna bora zaidi ya kuboresha
utendaji kazi katika wizara.
Aidha, Profesa Mchome alizungumzia umuhimu wa kuboresha Muundo wa Wizara
hiyo ili kuwezesha namna bora ya kutekeleza majukumu yake baada ya
ugatuaji wa uendeshaji na usimamizi wa shule za Sekondari kwenda kwenye
Halmashauri chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI na kwa kufuata Hati
Idhini iliyounda Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliyotolewa na
Mheshimiwa Rais, Desemba 2010.
Saturday, 19 July 2014
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment